
Watu watatu wanaosadikiwa kuwa
vinara wa kutengeneza vyeti bandia pamoja na nyaraka mbalimbali za Serikali
wamekamatwa eneo la Buguruni wakiwa na mitambo yao.
Kukamatwa kwao kulitokana na msako
mkali uliofanywa na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam hivi
karibuni na hatimaye watuhumiwa walinaswa wakiwa nyumbani wanakoishi eneo la
Buguruni Ghana wakitengeneza nyaraka bandia.
Kamanda wa kanda hiyo, Simon Sirro
aliwataja watuhumiwa waliokamatwa kuwa ni Ashraff Maumba (37) mkazi wa Buguruni
Ghana, Mwamba Seif (38) mkazi wa Mnyamani, na Mahmudu Zuber (24) mkazi wa
Buguruni.
Sirro aliwaambia waandishi wa
habari jana kwamba Julai 8, saa 4.00 usiku walifanya upekuzi katika nyumba
wanayoishi na kukuta nyaraka mbalimbali vikiwamo vyeti bandia vya kidato cha
nne 50 na vyeti vya vyuo vya uuguzi.
Kamanda huyo alisema nyaraka
nyingine bandia zilizokamatwa ni stika 20 za Mamlaka ya Usafirishaji wa Majini
na Nchi Kavu (Sumatra), vyeti vya kuzaliwa 10 na vya Chuo cha Ufundi (Veta).
Nyaraka nyingine zilizokamatwa, kwa
mujibu wa Sirro ni leseni za biashara, stika 100 za bima za magari, mitambo na
vivuli 10 bandia vya vyeti vya Chuo cha Biashara (CBE).
Katika upekuzi huo pia walikamata
mihuri mbalimbali ya ofisi za Serikali na binafsi ukiwemo muhuri wa Bibi na
Bwana.
“Tulifanikiwa kukamata vifaa
mbalimbali vya kutengenezea nyaraka zikiwamo karatasi maalumu zilizo na nembo
ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa ajili ya kutengeneza zaidi ya kadi 500
za vyombo vya moto, kompyuta nne na mashine moja ya kuchapisha,” alisema Sirro.
Kamanda Sirro alisema
watuhumiwa wanashikiliwa na Jeshi la Polisi huku upelelezi ukiendelea na
ukikamilika watafikishwa mahakamani ili kujibu mashtaka yanayowakabili.
Katika hatua nyingine, Mpiga Chapa
Mkuu wa Serikali, Cassian Chibogoyo alisema Serikali haitakubali kuhujumiwa na
watu wachache hivyo itachukua hatua kali kwa wote wanaojihusisha na
utengenezaji vyeti bandia vya Serikali.
“Tunashukuru jeshi la polisi kuibua
shina ambalo lilikuwa linatusumbua sana kutambua ni wapi wanatengeneza vyeti hivi
vya bandia na tumepata taarifa za mawakala wanaofanya ujanja huo,” alisema
Chibogoyo.

No comments:
Post a Comment