Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli jana tarehe 30 Julai, 2016 ameendelea na ziara
yake katika Mkoa wa Tabora akitokea Mkoa wa Singida.
Kabla ya kuingia Mkoani
Tabora, Rais Magufuli amezungumza na wananchi wa Mji wa Misigiri katika Wilaya
ya Iramba ambapo amemuagiza Meneja wa Wakala wa Barabara katika Mkoa wa Singida
kuhakikisha mkandarasi anayejenga daraja la Sibiti anarejea kazini mara moja
kukamilisha ujenzi wa daraja hilo.
Rais Magufuli amesema serikali yake
imejipanga kumlipa fedha mkandarasi huyo na hivyo hakuna sababu ya kuendelea
kusimamisha ujenzi huo.
Mkoani Tabora, Rais Magufuli
amezungumza na wananchi waliosimamisha msafara wake katika vijiji vya Nanga na
Ziba na amefanya mikutano ya hadhara katika miji ya Igunga na Nzega ambako
amewahakikishia wananchi kuwa serikali yake itahakikisha inatekeleza ahadi
zilizopo katika Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya Mwaka 2015.
Katika mkutano wa hadhara
uliofanyika Igunga, Rais Magufuli amepokea malalamiko ya wananchi kuhusu
kutoanza kutumika kwa kituo cha mabasi na soko na amewaagiza viongozi wa Mkoa
wa Tabora kuhakikisha kituo cha mabasi cha Igunga na soko la Igunga vinaanza
kutumika kuanzia Jumatatu ijayo ya tarehe 01 Agosti, 2016.
Kuhusu kero ya maji, Dkt. Magufuli
amesema Tanzania imepata mkopo wa dola za kimarekani Milioni 268.35 kutoka
nchini India ambazo zitatumika kutekeleza mradi wa kusambaza maji ya ziwa
Viktoria katika Miji ya Tabora, Igunga, Nzega, Sikonge na Uyui pamoja na
vijiji vilivyopo kandokando mwa bomba kuu kuanzia mwaka huu ambapo watu milioni
moja na laki moja (1,100,000) watanufaika.
Dkt. Magufuli ameongeza kuwa pamoja
na juhudi hizo Serikali imefanya usanifu na upembuzi yakinifu kwa ajili ya
kutekeleza mradi wa kusambaza maji ya kutoka mto Malagarasi kwa ajili ya Miji
ya Urambo, Kaliua na Nguruka pamoja na vijiji vilivyopo kandokando mwa bomba
kuu ambako watu laki sita (600,000) watanufaika.
Aidha, Rais Magufuli amepiga
marufuku wakulima wadogo kutozwa ushuru wa mazao watokapo na mazao mashambani.
“Ninapenda tukusanye kodi, lakini
sio kukusanya kodi kutoka kwa watu masikini, mtu ametoka shambani na magunia
yake mawili au hata matano halafu nyinyi mnamtoza kodi.
“Mimi sipendi kuwanyanyasa hawa
watu wanyonge, mtu akiwa na mazao lori zima hapo sawa lakini sio kwa mtu
mnyonge mwenye gunia moja” Amesema Rais Magufuli.
Kuhusu maombi ya Mkoa wa Tabora
kutaka kuanzishwa Mkoa mwingine kutokana na ukubwa wa baadhi ya Wilaya Rais
Magufuli amesema haoni umuhimu wa kuanzisha Mikoa mipya hapa nchini kwa sasa,
na badala yake fedha zitaelekezwa katika huduma kwa wananchi kama vile maji,
barabara, miundombinu na huduma za afya.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano,
IKULU
Nzega
30 Julai, 2016
No comments:
Post a Comment