Mgombea urais wa chama cha Republican nchini Marekani Donald
Trump amemchagua Mike Pence kuwa mgombea mwenza, taarifa katika vyombo vya
habari Marekani zinasema.
Maafisa wa kampeni wa Bw Trump walipanga atangaze uamuzi wake
Ijumaa, lakini hafla hiyo ikaahirishwa kutokana na shambulio la kigaidi
lililotokea Nice, Ufaransa.
Duru za karibu zimeambia shirika la habari la ABC News kwamba Bw
Pence amekubali kuwa mgombea mwenza.
Hata hivyo, Bw Trump aliambia Fox News Alhamisi jioni kwamba:
“Bado sijafanya uamuzi wangu wa mwisho, uamuzi wa mwisho.”
Wachanganuzi wanasema Bw Trump atatumaini bw Pence atamsaidia
kuwavutia wahafidhina katika chama chake.
Wagombea wengine ambao walipigiwa upatu kuchaguliwa na Bw Trump
kuwa mgombea mwenza ni Spika wa Bunge Newt Gingrich na Gavana wa New Jersey
Chris Christie.
Bw Pence ni gavana wa Indiana na mwanachama wa vuguvugu
la siasa za mrengo wa kulia la Tea Party.
Akiteuliwa, basi Bw Pence atakuwa
makamu wa rais wa Bw Trump iwapo atafanikiwa kumshinda mgombea wa chama cha
Democratic Hillary Clinton kwenye uchaguzi mkuu Novemba.

No comments:
Post a Comment