Vikongwe wawili mke na mumewe wa
Kitongoji cha Nyag’holongo, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, wameuawa kwa
kutumia silaha za jadi na watu wasiojulikana wakituhumiwa kuwa ni wachawi.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Geita, Isack Msengi alisema tukio hilo lilitokea Julai 22 saa tatu usiku
nyumbani kwao.
Aliwataja wanandoa hao kuwa ni
Machene Magina (80) na Mkewe Genke Bundara (75) ambao waliuawa na wananchi
wakiwatuhumu kwa uchawi.
Msengi alisema watu watano wanashikiliwa
na polisi na upelelezi wa tukio hilo bado unaendelea. Diwani wa Kata ya Nanda,
Jumamosi Mathias alisema kundi la watu ambalo halijulikani lilivamia nyumbani
kwa familia hiyo wakati wakijiandaa kulala na kufanya ukatili huo.
Mathias alisema akiwa nyumbani
kwake, alisikia kelele za watu wakisema; “Tumechoshwa na hawa wachawi.
Kwa kuwa hawa wazee ni majirani zangu, nilianza kuhangaika ili kuona jinsi ya
kudhibiti maafa hayo,” alisema Mathias.
Hata hivyo, alisema kabla ya
kutoa taarifa polisi, watu hao waliivamia nyumba hiyo na kufanya mauaji hayo ya
kinyama kwa vikongwe hao.
Alilaani kitendo kilichofanywa na
watu hao kuwa ni cha kikatili dhidi ya wazee kwani tangu aishi nao kijijini
hapo hakuwahi kusikia tuhuma za uchawi dhidi yao.
Mathias alitoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kuwahisi wazee kuwa ni wachawi na kujichukulia sheria mkononi, badala yake wawathamini na kuwalinda kwani wazee ni hazina ya Taifa.
Mathias alitoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kuwahisi wazee kuwa ni wachawi na kujichukulia sheria mkononi, badala yake wawathamini na kuwalinda kwani wazee ni hazina ya Taifa.

No comments:
Post a Comment