
KATIKA kutekeleza agizo la Rais
John Magufuli la kutaka serikali kuhamia Dodoma, Waziri wa Kilimo, Mifugo na
Uvuvi, Dk Charles Tizeba amesema watendaji wa wizara hiyo wataanza kuhamia
Dodoma kuanzia wiki ijayo.
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu
wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa amewataka wakuu wa
idara na vitengo wote wa wizara hiyo kuanza maandalizi ya kuhamia Dodoma na
kuwa wametekeleza agizo hilo ifikapo mwezi Septemba, mwaka huu.
Akizungumza jijini Dar es Salaam
jana, Dk Tizeba alisema tayari watendaji wa wizara hiyo wanaotakiwa kuhamia
Dodoma wameanza kufanya maandalizi ya safari.
Alitoa dokezo hilo mara baada ya
kutoa taarifa kuhusu Mkutano wa Ushirikishwaji wa Wadau kwenye Sekta ya Uvuvi,
unaoishirikisha pia Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi ya Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar na wadau mbalimbali.
“Ni kweli hata sisi Wizara tuko
kwenye maandalizi wiki hii, kwa sababu wiki ijayo tutahamia Dodoma,
tunatekeleza agizo la Rais,” alisema Waziri Tizeba.
Kauli ya Waziri Tizeba imekuja siku
moja baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kutangaza kuhamia Dodoma ifikapo
Septemba mwaka huu, huku akiwataka Mawaziri na Naibu Mawaziri kumfuata.
Waziri Mkuu alisema ameshaagiza
ukarabati kwenye nyumba yake ukamilishwe ili ifikapo Septemba aweze kuhamia na
kuwataka mawaziri kufanya hivyo kwa sababu kila Waziri ana nyumba na ofisi
ndogo mjini Dodoma.
Nayo Wizara ya Nishati na Madini
imetoa waraka ikiwataka wakuu wa idara na vitengo wote wa wizara hiyo kuanza
maandalizi ya kuhamia Dodoma ifikapo mwezi Septemba mwaka huu.
Agizo hilo lipo katika waraka
uliotolewa na Kabibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin
Ntalikwa jana na nakala yake kutumwa pia kwa Waziri wa Nishati na Madini,
Profesa Sospeter Muhongo.
Katibu Mkuu huyo alisema agizo hilo
linatokana na kauli iliyotolewa na Rais Magufuli katika Mkutano Mkuu Maalumu wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM) uliofanyika mjini Dodoma hivi karibuni, ambapo
alisisitiza azma ya serikali yake kuhamia Dodoma.
Alisema pamoja na kauli ya Rais,
watendaji hao wanatakiwa kuanza maandalizi ya kuhamia Dodoma ifikapo Septemba
kutokana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuahidi kuhamia Dodoma mwezi huo na
kuwataka Mawaziri na Naibu Mawaziri nao kumfuata.

No comments:
Post a Comment