
SERIKALI imeanza mkakati mpya wa
kuandikisha wananchi waliopo kwenye vijiji na vitongoji kwa njia ya
kielektroniki ili kupata takwimu sahihi zitakazosaidia utoaji wa huduma bora
kwa jamii.
Pia mfumo huo utatambua watu
wadanganyifu ambao wamekuwa wakidanganya wanakotoka, ikiwemo wezi na majambazi
ambao ni lazima waeleze wanakoishi, wanakotokea, jina la mkuu wa kaya wake na
namba ya utambulisho wake.
Mfumo huo ambao utasaidia kujua
watoto waliozaliwa na watu waliokufa, taarifa zitakazotolewa kwa Mtendaji wa
Serikali za Mitaa ambaye atarekodi kwa njia ya simu na taarifa hizo zitafika
moja kwa moja kwenye Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ambao wataweka kumbukumbu.
Akizungumza na waandishi wa habari
jana Dar es Salaam, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (TAMISEMI), Mussa Iyombe alisema kuwa ili kufanikisha uhakiki huo,
serikali imetenga Sh bilioni 1.6 wakati wahisani wamechangia Sh bilioni 1.4.
Iyombe alisema takwimu hizo pia
zitaisaidia Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na Wakala wa Udhamini na
Ufilisi (RITA) katika utoaji wa vitambulisho na hati za kuzaliwa na vifo.
Aidha, alisema lengo ni kuhakikisha kila mtu anatumia kitambulisho kimoja pekee
kumtambulisha kuliko ilivyo sasa kwamba watu wanakuwa na vitambulisho zaidi ya
saba.
"Hii itakuwa dawa ya
kuwatambua majambazi, wezi, wahamiaji wa kigeni na hata watoto wanaozaliwa na
vifo. Mtendaji wa mtaa atakuwa anarekodi taarifa hizo kutoka kwa mkuu wa kaya
ambapo ataeleza watoto waliokuwepo, wapangaji wangapi. Mpangaji pia akitaka
kuhama ni lazima aseme anakwenda wapi ili aweze kupokelewa anakokwenda,"alisema Iyombe.
Kwa mujibu wa Iyombe, awali
walikuwa wanatumia madaftari katika kusajili watu waliopo kwenye vijiji na
vitongoji hali ambayo ilikuwa na changamoto kutokana na watendaji wengine
kutojaza taarifa za wakazi wao.
Alisema kuwa serikali imekuwa
ikikosa taarifa muhimu za awali na kuamua kuanza mfumo huo ambao utafanyika
nchi nzima kwa miaka miwili.
Aliongeza kuwa kwa kushirikiana na
Chuo cha Takwimu Kusini mwa Afrika waliamua kuanza mfumo huo Kata ya Mapinga
wilayani Bagamoyo na kwamba wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa.
Alisisitiza kuwa sensa ya mwaka
2022 itatumia taarifa zitakazokusanywa kwa kipindi cha miaka miwili ijayo ili
kuondoa ubabaishaji uliokuwa unafanywa awali.
Pia alisema kwa sasa nchi
inapopatwa na janga lolote hutumia taarifa zisizo rasmi kwa ajili ya kutoa
msaada, hivyo vijiji vingine kuona kuwa serikali haiwasaidii wanapopatwa na
matatizo.
Kwa upande wake, Kamishna wa Sensa
ya Watu na Makazi, Amina Said alisema kuwa kabla ya sensa nyingine Tamisemi
wawe wamemaliza uhakiki wa watu kutumia mfumo huo.
Alisema kuwa katika nchi
zinazotumia mfumo huo, hakuna sensa kwa kuwa wanazo taarifa sahihi za watu wao.
"Mfumo huu utaingiza
watu wapya na kuwatoa waliokufa ili kufanya makadirio mazuri yatakayosaidia
kuwatambua watu wote ikiwemo wavamizi pia itapunguza muda wa kupata idadi ya
watu," alisema Said.
Pia alisema kuwa wasimamizi wakubwa
wa mfumo huo ni Tamisemi hivyo wananchi washirikiane na viongozi wao kutoa
taarifa sahihi ili kuwatambua na si kwa nia mbaya.
Hata hivyo alisema kuwa kupitia
mfumo huo itasaidia wanafunzi kuandikishwa kwenye shule zilizopo maeneo yao
kuliko kuandikisha watoto nje ya kata ya mwanafunzi.
Aliwataka wanasiasa na viongozi
wote watambue na kushiriki katika kuwaelimisha wananchi na kuwatoa hofu kuhusu
mfumo huo ili kutoa huduma bora za jamii.
Naye, Diwani wa Kata ya Mapinga
Bagamoyo ambaye kata yake imefanyiwa majaribio, Ibrahim Mbonde alisema kuwa
ameandikisha kaya 341 kwa njia ya kielektroniki na kwamba mfumo umeonesha
mafanikio makubwa.
Mbonde alisema serikali imeondoa
gharama za kununua madaftari kwa ajili ya uhakiki ambavyo vilikuwa havijazwi.
Alisema walikuwa wanashindwa kupata taarifa za watu ikiwemo wajawazito
wanaojifungulia nyumbani na wanaokufa na kusababisha kuwepo kwa takwimu za
kukisia.
"Kila kaya inakuwa na namba
yake hivyo mtu anayeenda kuhakiki na kutaja namba tofauti hutambulika kuwa
mdanganyifu. Kwa mfano kwangu watu wapo 23,000 ni lazima tungenunua madaftari
mengi, njia hii itasaidia kuleta maendeleo ya Taifa," alisema Mbonde.

No comments:
Post a Comment