Serikali imetakiwa kufanya
marekebisho ya sheria mbalimbali ambazo zimeonekana kuwa kandamizi ikiwepo ile
sheria za vyombo vya habari ambazo zinakandamiza uhuru wa vyombo vya habari
pamoja na waandishi wenyewe.
Akitoa ripoti ya nusu mwaka mbele
ya wanahabari kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Mkurugenzi wa kituo cha
sheria na haki za binadamu Bi Hellen Kijo Bisimba amesema kuwa vyombo vya
habari havifanyi kazi kwa uhuru kwani zipo sheria ambazo bado ni kandamizi.
”Vyombo vya habari bado havina
uhuru kwani sheria kandamizi bado zinatumika mfano, gazeti la mawio kufungiwa
na kutakiwa kutoandika nakala zake hata kwenye mitandao bila sababu maalumu”.Ilielezwa katika
ripoti ya kituo hicho
Aidha ripoti hiyo ya miezi sita
imesema kuwa wananchi bado wananyimwa haki zao za msingi ikiwa ni pamoja
na kunyimwa haki ya habari kwasababu serikali imeamua kutorusha
matangazo ya bunge kwa sababu mbalimbali ambazo zinakinzana.
Katika ripoti hiyo pia imegusa haki
za kujumuika ambapo kituo hicho kimesema matamko ya jeshi la polisi hasa katika
kuzuia mikutano ya vyama imeonekana kupendelea chama tawala huku vyama
vya upinzani vikiwa vinakandamizwa.
”Mfano mkutano wa Chadema shinyanga
ulipewa vibali vyote lakini baadae ukaja kutawanyishwa kwa kutumia nguvu mpaka
mabomu, aidha ACT walikuwa na kongamano la kuchambua bajeti lakini jeshi la
polisi walizuia lakini wakati huo huo CCM walikubaliwa kufanya mkusanyiko” Ilieleza
semu ya ripoti ya Kijo Bisimba.
Pamoja na hayo ripoti hiyo imetoa
mapendekezo kwa Serikali ikiwa kuboresha sheria hizo kandamizi kwa
wananchi pamoja na kuachia vyombo vya habari kufanya kazi zake pasipo
kuingiliwa sambamba na Vyama vya siasa kupewa haki sawa.

No comments:
Post a Comment