
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) Kanda ya Dar es Salaam, kimemkaribisha Kamanda wa Polisi wa Kanda
hiyo, Kamishna Simon Sirro kujitokeza na kuwa mstari wa mbele kwenye maandamano
ya Operesheni Ukuta yatakayofanyika Septemba Mosi.
Kimesema kinamkaribisha kamanda
huyo ili kuondoa uwezekano wa kupelekewa taarifa za uongo na askari wake kuhusu
maandamano hayo.
Makamu Mwenyekiti wa Chadema Kanda
ya Dar es Salaam, Benard Mwakyembe, alisema jana kuwa hakuna haja ya kamanda
huyo kukaa ofisini bali ajitokeze katika Operesheni Ukuta na awe mstari wa
mbele kuwapiga wananchi ambao watatumia muda huo kumuuliza maswala ya sheria
kuhusu maandamano hayo.
“Lengo la Operesheni Ukuta ni
kuwaeleza wananchi kuwa nchi yetu haifuati sheria bali inafuata mawazo ya mtu
mmoja.
“Tumwambie tu kwamba Kamanda Sirro
ngoma hii ya Ukuta si ya kitoto, vitisho na mbwembwe zake anazozionyesha
barabarani hazitutishi, tupo tayari kwa lolote.
“Tumejiandaa kisaikolojia kwa namna
yoyote, tupo tayari kufa kwa ajili ya kuwatetea wananchi, na Meya wa Jiji la
Dar es Salaam, Isaya Mwita, atakuwa mstari wa mbele pamoja na viongozi
wengine,” alisema Mwakyembe.
Aidha alisema maandalizi yote
yamekamilika kwa asilimia 99.5 katika mitaa 582 na kata 102 ya jiji zima la Dar
es Salaam.
“Niwashukuru Umoja wa Vijana wa
Chama Cha Mapinduzi (UV-CCM) kwa kutuunga mkono kuandaa maandamano yao,
tunaamini haya ya kwetu yamewapa motisha na kuamua kufanya ya kwao.
“Ninaliomba Jeshi la Polisi liwape
ulinzi wa kutosha ingawaje sisi tunajua kwamba huo ni mtego walioufanya kisiasa
ili kuleta mabishano ambayo hayana nafasi kwetu,” alisema.
Alisema haki za vyama vya siasa ni
kutoa maoni ya kisiasa kadiri vitakavyoona inafaa, ili kutekeleza sera
zake kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania na Katiba ya Zanzibar.

No comments:
Post a Comment