
MKE wa bilionea Erasto Msuya, Miriam Elisaria Msuya (41)
amefikishwa mahakamani kwa tuhuma za mauaji ya dada wa wa bilionea huyo, Aneth
Msuya.
Mshtakiwa huyo alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu jana jijini Dar es Salaam na kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali,
Diana Lukondo mbele ya Hakimu Mkazi, Margareth Bankika.
Akisoma mashtaka hayo, Lukondo alidai mshtakiwa huyo ambaye ni
mkazi wa maeneo ya Sakina kwa Iddi, jijini Arusha anadaiwa Mei 25, mwaka huu
katika maeneo ya Kibada Kigamboni jijini Dar es Salaam alimuua Aneth Elisaria
Msuya.
Mshtakiwa hakutakiwa kujibu lolote kwa sababu mahakama hiyo haina
uwezo wa kusikiliza kesi za mauaji, mbapo Jamhuri ilidai upelelezi
haujakamilika na kuomba kesi hiyo ipangwe tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Hakimu Bankika, alikubali kuahirisha kesi hiyo hadi Septemba 9,
mwaka huu kwa ajili ya kutajwa na mshtakiwa alirudishwa rumande.
Habari zilizopatikana baada ya tukio hilo zilidai kwamba,
marehemu Aneth aliuawa kwa kuchinjwa na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia Mei
25, mwaka huu Dar es Salaam.
Mauaji hayo yalitokea nyumbani kwake eneo la Kibada block 16,
Kigamboni ambako inaelezwa wauaji hao hawakuchukua kitu chochote ndani ya
nyumba yake.
Marehemu Erasto Msuya, aliyekuwa mfanyabiashara wa madini ya
Tanzanite aliuawa kwa kufyatuliwa risasi Julai 7, mwaka 2013 katika eneo la
Mijohoroni, kando ya barabara ya Arusha – Moshi wilayani Hai mkoani
Kilimanjaro, akiwa ameitika wito wa kwenda kununua madini ya Tanzanite baada ya
kupigiwa simu na vijana wawili waliomtaka wakutane maeneo hayo.
Inaelezwa kuwa alifika katika eneo hilo akiwa na gari lake aina
ya Range Rover T 800 CKF na kuwakuta vijana hao wakimsubiri, baada ya kuteremka
Msuya alielekea kumsalimia mmoja wa vijana hao.
Hata hivyo kabla hajamfikia kijana huyo aliitoa bunduki ya SMG
namba KJ 10520 aliyokuwa ameificha kwenye koti na kumfyatulia risasi takribani
22 mwilini.

No comments:
Post a Comment