
Aliyekuwa Waziri wa Kilimo na Chakula na Kada mkongwe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Stephen Wassira ameomba wasaidizi wa Rais John Magufuli kumshauri kufanya mazungumzo na viongozi wa upinzani ili kuepusha madhara yanayoweza kutokea kutokana na maandamano yanayopangwa kufanyika Septemba 1.
Wassira ameeleza kuwa washauri hao
wanapaswa kufanya hivyo kwani bado nafasi hiyo ipo kuliko kuacha Rais aingie
vitani na wananchi wake kwani madhara yatawapata Watanzania wote.
“Wazungumze ili
wasimuingize Rais kupigana na watu wake kwa maana wote tutapoteza. Kwa nini
uweke askari polisi wote hao, msimweke Rais kwenye vita na watu wake,” Wassira
anakaririwa na Jambo Leo.
“Kinachohitajika
ni wasaidizi wa Rais kumshauri ili kuhakikisha kuwa tofuati zilizopo baina yake
na vyama vya upinzani haziendelei ili kuepusha madhara yanayoweza kuzuilika,
itafutwe suluhu,” aliongeza.
Akizungumzia uamuzi wa Serikali
kupiga marufuku kufanyika kwa mikutano na maandamano, alisema kuwa tatizo
linaweza kuwa ni aliyekuwa Mgombea wa Urais kwa tiketi ya Chadema, Edward
Lowassa.
Alisema kuwa hii inatokana na joto
la uchaguzi lililokuwepo pamoja na nia ya Lowassa kuzunguka nchi nzima
kuwashukuru wapiga kura, kungeweza kuzua tafrani kubwa kwani alipata kura
nyingi na alikuwa akidai ameshinda kwa asilimia 62.
“Ukiwaruhusu
kufanya mikutano na ukwaambia kuwa atakayekuja kutoa shukurani ni Lowassa,
ambaye amekuwa akipinga kushindwa ni sawa na kurejesha hali ya uchaguzi kipindi
hiki,” alisema.
Alitaka Serikali kutoa elimu ya
wazi kwa umma kuhusu sababu zinazopelekea kukataza kufanyika kwa mikutano ili
kuweka mambo sawa.
“Kama mimi hapa
nimetaja sababu kwamba inawezakana kuwa ni Lowassa. Sasa na wao Serikali waseme
tu tunapiga marufuku mikutano na maandamano… wataje [sababu]na kuzifafanua,” alieleza.
Hata hivyo, Wassira aliwataka
Chadema kusitisha adhma yao na kuhakikisha wanafuata utaratibu ili kupata haki
ya kufanya maandamano na mikutano ambayo alieleza kuwa kila Katiba ya nchi
duniani imeiweka, lakini bila kufuata utaratibu haiwezi kuruhusiwa.

No comments:
Post a Comment