Mwenyekiti wa Chadema, Freeman
Mbowe, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama hicho, Edward Lowassa na viongozi wengine
waandamizi wameitwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwenda
kuripoti kesho Septemba Mosi.
Hatua hiyo inatokana na viongozi
hao kukamatwa juzi, baada ya kufanya mkutano maalumu wa ndani wa Kamati Kuu, na
walipelekwa Kituo Kikuu cha Polisi cha Kanda hiyo na kuhojiwa kabla ya
kuachiwa.
Mbali na Mbowe na Lowassa, viongozi
wengine wa Chadema waliokamatwa na kutakiwa kwenda Polisi kesho ni Katibu Mkuu,
Vincent Mashinji, Naibu wake, John Mnyika na Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho,
Said Issa Mohammed.
“Wameitwa Polisi waende Septemba
mosi kuripoti baada ya jana kukamatwa na kuhojiwa wakituhumiwa kukiuka maagizo ya
Polisi,”alisema Msemaji wa Chadema, Tumaini Makene na kufafanua:
“Lakini wanaweza kwenda au
wakaanzia kwenye maandamano kisha wakaenda Polisi kuripoti.”
Alisema maandamano hayo yatakuwapo
kama yalivyopangwa kwani maandalizi yake yamekamilika.
Habari zaidi zilieleza, kwamba jana
mchana viongozi hao walikuwa wakifanya kikao Makao Makuu ya chama hicho
Kinondoni Dar es Salaam, ambapo pia walikutana na wabunge wote wa chama hicho
kwa makundi tofauti.
Kwa mujibu wa mtoa habari ndani ya
Chadema makao makuu katika kikao hicho walijadili mambo mengi ikiwa ni pamoja
na suala la utekelezaji wa Ukuta kesho.
Mmoja wa wabunge wa Chadema
alisemai kwamba walikuwa wakiwekana sawa kuhusu maandamano yao.
Alibainisha kwamba katika mkutano
huo ambao Mbowe hakuwepo pia walijadili maombi ya viongozi wa dini kuwataka
kusitisha maandamano hayo Septemba mosi.
“Viongozi wa dini wamekuwa
wakituomba tusitishe maandamano ya Ukuta Septemba mosi, tusubiri hadi baada ya
mkutano wa vyama vya siasa Septemba tatu,” alisema Mbunge huyo wa Kanda
ya Ziwa.
Aliongeza: Katika mkutano
huo, Lowassa na viongozi wengine walijadili hayo na ikikubalika kwa heshima ya
viongozi wa dini maandamano ya Ukuta yafanyike baada ya Septemba tatu.”
Hata hivyo, mwandishi
alishuhudia wabunge wengi wa chama hicho wakitoka katika mkutano huo kimya
kimya bila kutaka kuzungumza na kabla muda uliopangwa kwisha, huku taarifa
zikieleza kwamba mkutano huo uliahirishwa baada ya kuwepo taarifa za kutaka
kuvamiwa na Polisi.
“Tumeambiwa tusambaratike,
tutajulishwa wapi tutakutana tena, kama hapa au wapi,” alidokeza mmoja
wa wabunge hao.
Baada ya mkutano huo kuahirishwa,
Lowassa alitoka eneo hilo huku taarifa zikieleza alikuwa akielekea kwenye moja
ya hoteli jijini humo kuungana na Mbowe ambapo walikuwa na mazungumzo na baadhi
ya viongozi wa dini.

No comments:
Post a Comment