Septemba mosi mwaka huu inataraji
kuingia katika histori ya Tanzania kutokana na matukio ambayo yanataraji
kufanyika siku hiyo, matukio hayo ni pamoja na sherehe za miaka 52 ya Jeshi la
Wananchi la Tanzania (JWTZ), maandamano ambayo yamepangwa kufanywa ya UKUTA na
tukio la kupatwa kwa jua.
Akizungumza na Waandishi wa Habari
wakati alipokutana na Maafisa wa Jeshi la JWTZ Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam, Paul Makonda alisema JWTZ inapotimiza miaka 52 ni fahari kubwa hivyo
tunapaswa kuwapongeza kwa kudumisha amani na mshikamano.
Alisema Jeshi hilo limejipanga
kurusha angani ndege zake za kivita katika anga la Dar es Salaam, Septemba 1
mwaka huu, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 52 ya kuanzishwa kwake.
Makonda aliwataka wananchi kutokuwa
na hofu wanaposikia ngurumo za ndege hizo bali wafurahie kwani ni ndege zao.
“Mnaposikia milio ya ndege zetu
mbalimbali, mfurahie kwa sababu hizo ni ndege za wananchi. Usisikie muungurumo
ukashtuka. Hakuna jambo lolote lile zaidi ya kuonesha vifaa vyetu na jinsi
ambavyo wanajeshi wetu kwa miaka 52 wamaeendelea kuwa imara na vifaa vizuri,” alisema
Makonda.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa waliwataka
wananchi waliojipanga katika vikundi mbalimbali kuripoti kwa wakuu wao wa
wilaya kujiandikisha ili waweze kushiriki pamoja na Jeshi hilo katika zoezi la
usafi jijini humo.
Aliwataka wakazi wa mkoa huo pia
kujitokeza kuchangia damu katika vituo mbalimbali ambavyo vimeanishwa ili
kuunga mkono juhudi za uchangiaji damu zitakazofanywa na wanajeshi wa JWTZ.
“Hii ni sehemu ya amani, tufanye
usafi kwa amani. Tujitolee damu zetu kwa amani na mwisho wa siku tuwaenzi na
kuwapongeza wanajeshi wetu kwa kazi kubwa wanayoifanya,” Makonda
alieleza.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa
Mkoa aliendelea kutoa onyo kwa watu watakaotaka kufanya maandamano yaliyopigwa
marufuku ya oparesheni UKUTA akiwataka kutii sheria.
“Mimi ninavyojua UKUTA ni kuwa mtu
amefika mwisho wa kufikiri sasa kama watakuwa wamefika mwisho wa kufikiria basi
sisi tutawasaidia … watu wapo wanapanga kufanya mambo ya kusaidia jamii wao
wanapanga maandamano nawashauri wananchi waungane na Polisi,”alisema Makonda.

No comments:
Post a Comment