MAMLAKA ya Kupambana na Rushwa na
Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA), imemhoji Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF),
Maalim Seif Sharif Hamad, baada ya kuwahusisha baadhi ya viongozi na watendaji
wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na tuhuma za ufisadi.
Ofisa wa Kitengo cha Elimu kwa Umma
cha ZAECA, Abubakari Mohamed Lunda, alisema jana kuwa Maalim Seif alihojiwa na
Mkurugenzi wa ZAEC, Mussa Haji Ali, ili athibitishe tuhuma hizo.
Lunda alisema tuhuma zilizotolewa
dhidi ya watendaji na viongozi ni nzito ndiyo maana mamlaka hiyo imeamua
kuchunguza ukweli wake kwa manufaa ya Zanzibar na wananchi wake.
Lunda alisema kazi kubwa ya mamlaka
hiyo ni kuchunguza jambo lolote ambalo linahusu maslahi ya Zanzibar katika
kupambana na vitendo vya rushwa na uhujumu uchumi.
“Tayari mamlaka
imemhoji Maalim Seif ili kutafuta ukweli juu ya tuhuma alizotoa za kuwapo
viongozi wanaomiliki fedha chafu na mali nje ya nchi,” alieleza
Lunda.
Alisema nia ya kumhoji Maalim Seif
ilikuwa kupata ukweli wa tuhuma alizotoa dhidi ya viongozi na watendaji
aliowatuhumu kwa kumiliki fedha chafu na mali nje ya nchi.
Hata hivyo, Lunda alisema mpaka
sasa hafahamu mkurugenzi amegundua kitu gani baada ya kufanyika kwa mahojiano
hayo huku akisisitiza kuwa ZAECA imetimiza wajibu wake wa kupokea na kuchunguza
taarifa mbalimbali wanazopata kupitia wanasiasa, vyombo vya habari na wananchi.
Lunda pia alisema kuna majalada 20
yamekabidhiwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar (DPP), Ibrahim Mzee kwa ajili
ya hatua za kisheria kuchukuliwa.
Alisema majalada hayo yanahusisha
kesi mbalimbali zikiwamo za rushwa ya uchaguzi zilizotokea wakati wa kura ya
maoni ya kuwapata wagombea wa ubunge na uwakilishi kupitia CCM mwaka jana.
Alisema kitendo cha majalada kukaa
muda mrefu kwa DPP bila ya kufunguliwa mashtaka mahakamani si jukumu la ZAECA
kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984.
"Ni jukumu
la Mkurugenzi wa Mashtaka wa Zanzibar (DPP)," alisema.
Akizungumza na waandishi wa habari,
Aprili 10 mwaka huu mjini Zanzibar, Maalim Seif, ambaye ni Makamu wa kwanza wa
Rais wa zamani wa Zanzibar alituhumu kuna viongozi na watendaji wa visiwani
humo wanamiliki fedha chafu na mali nje ya nchi.
Alisema kuwa fedha hizo
zilipatikana kwa njia za ufisadi na kutaka jumuiya ya kimataifa kufuatilia
akaunti za vigogo hao na watendaji nje ya nchi kwa manufaa ya Zanzibar na
wananchi wake.
Maalim Seif alidai kuwa haihitajiki
tochi kuwamulika viongozi wanaokabiliwa na tuhuma za ufisadi na kutaka mamlaka
za dola kufanya uchunguzi dhidi ya vigogo hao na kuchukua hatua kwa mujibu wa
sheria.

No comments:
Post a Comment