MWANASHERIA Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu amesema licha ya viongozi wa chama hicho kutishwa, kukamatwa na kuhojiwa na Jeshi la Polisi, bado msimamo wao kuhusu operesheni Ukuta itakayofanyika Septemba Mosi mwaka huu uko pale pale.
Chama hicho kinatarajiwa kufanya
operesheni mpya iliyopewa jina la Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania
(Ukuta).
Operesheni hiyo inatarajiwa kuwa
itakwenda sambamba na uzinduzi wa mikutano ya hadhara nchi nzima, ambayo
itafanyika Septemba Mosi, mwaka huu.
Hatua hiyo imefikiwa na kikao cha
Kamati Kuu ya chama hicho iliyoketi kwa siku nne mfululizo wiki iliyopita
jijini Dar es Salaam na kutoa maazimio matatu ambayo yatatekelezwa na chama
hicho.
Pamoja na mambo mengine, chama
hicho kimesema lengo la operesheni hiyo ni kuzuia matukio ya ukandamizaji wa
haki na demokrasia nchini, kiliyodai kuwa yanafanywa na Rais Dk. John Magufuli.
Akizungumza na waandishi wa habari
jana jijini Dar es Salaam baada ya kuhojiwa na kuachiwa kwa dhamana Mwenyekiti
wa Chadema, Freeman Mbowe, Mwanasheria Lissu alisema msimamo wao uko
palepale na hakuna kilichobadilika.
“Wamemuhoji kwa taarifa aliyoitoa
mbele ya waandishi wa habari juu ya msimamo wa chama wa kufanya mkutano nchi
nzima. Tatizo jeshi letu wakisikia maandamano, mkutano au mtu anamsema Magufuli
basi anatuhumiwa kwa uchochezi, wametumia muda mrefu kumuhoji lakini mwisho
wamemwachia kwa dhamana na amewahi ‘Airport’ ili aende kuhudhuria mazishi ya
kamanda wetu Senga (Joseph) na watamwita watakapomwihitaji tena,” alisema Lissu.
Alisema pamoja na hayo bado msimamo
wa chama hicho kufanya mikutano waliyoiita Operesheni Ukuta ipo pale pale
ifikapo Septemba Mosi, mwaka huu.
“Nafikiri ni muhimu sana huko
tunapoenda kuzungumza na wenzetu hii kitu inaitwa uchochezi ni nini?
Tunashitakiwa kwa sheria ya magazeti ya mwaka 1976 ambayo waliingiza vifungu
vya uchochezi mwaka 1978 lengo lao kuu ni kuwafunga watu midomo na ilitungwa
wakati wa mfumo wa chama kimoja.
“Hata hivyo Hayati Baba wa Taifa,
Mwalimu Julius Nyerere ndiye wa kwanza kushtakiwa kwa uchochezi pamoja na
mwandishi Robert Makenge na mwenzao Rashid Bagedae, kwa msingi huo sisi
tunafuata nyayo zake,” alisema.
Lissu ambaye pia ni Mbunge wa
Singida Mashariki (Chadema), alisema kuitwa mchochezi, ni jambo la ufahari
kupinga udikteta kama alivyokuwa Mwalimu Nyerere.
“Nasema hivyo kwa sababu Mwalimu
Nyerere ndiye wa kwanza kuitwa mchochezi, ni kitendo cha kufunga watu midomo
ili washindwe kuwaita watu wajinga pale wanapofanya ujinga.
“Tume ya Jaji Nyalali mwaka 1992
wakati mfumo wa vyama vingi unatambulishwa na kuanza nchini ilipendekezwa
sheria hii ifutwe kwa sababu haiendani na mfumo uliopo lakini hakuna
kilichofanyika,”alisema.
Mwanasheria huyo ambaye naye
amefunguliwa kesi ya uchochezi katika Mahakama ya Kisutu jijini Dar, aliwataka
wafuasi wa chama hicho kujitokeza kwa wingi Agosti 2, mwaka huu mahakamani hapo.
“Dawa yao si majaji bali umma… umma
ufurike, tutawashinda hawa watu makesi yenyewe ni haya ambayo hayana
kichwa wala miguu,”alisema na kushangiliwa na wafuasi wa chama hicho.
Mbowe alifika kituoni hapo akiwa
ameongozana na viongozi mbalimbali wa Chadema akiwamo Waziri Mkuu Mstaafu,
Edward Lowassa ambaye hata hivyo alizuiwa kuingia katika chumba cha mahojiano.
Askari waliokuwa kwa wingi katika
eneo hilo, walisikika wakisema kuwa anayepaswa kuingia ndani ni Mbowe,
Mwanasheria Tundu Lissu na Wakili wa Chadema, John Mallya.
Lowassa, wafuasi wa Chadema na
waandishi wa habari walilazimika kubaki nje huku askari wakiimarisha ulinzi
wakiwa wamebeba bunduki zao huku magari yenye maji ya kuwasha yakiwa
yameegeshwa pembeni.
Wakati chama hicho kikijiandaa
kutekeleza Operesheni Ukuta Septemba Mosi, tayari Rais Magufuli amezuia
operesheni hiyo na kuwaonya wale wote watakaokaidi agizo lake na kuamua
kuandamana.
No comments:
Post a Comment