Mkurugenzi wa Sheria wa Chadema, Peter Kibatala amempa pole aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Azimina Mbilinyi kwa kuenguliwa kwenye nafasi hiyo, ikiwa ni siku moja baada ya kesi za uchaguzi alizotolea ushahidi wilayani Kilombero kuhukumiwa.
Akiandika katika ukurasa wake wa
Facebook jana, Kibatala alisema:“Tunasikitika nawe, na kukupa pole nyingi
sana.”
Katika ujumbe huo aliothibitisha
baadaye kuuandika, Kibatala aliongeza:“Tunakushukuru sana kwa kutoa ushahidi
wa ukweli na wa haki katika kesi za uchaguzi majimbo ya Kilombero na Mlimba
yaliyotolewa hukumu jana (Julai 29).”
Wakili hiyo aliongeza: “Wakati wa Uchaguzi Mkuu ulikuwa Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Kilombero na Msimamizi wa Uchaguzi katika Majimbo waliyoshinda
Chadema.”
Juzi, taarifa ya Ofisi ya
Rais–Tamisemi iliyotolewa na Katibu Mkuu, Mussa Iyombe bila kufafanua
sababu za kuenguliwa kwake, ilieleza kwamba Rais John Magufuli ametengua uteuzi
wa Mbilinyi kwa sababu hakuridhishwa na utendaji wake wa kazi.
Mbilinyi alikuwa mkurugenzi wa
Halmashauri ya Kilombero kabla ya kuhamishiwa Dodoma na baadaye Bagamoyo.
Alipotafutwa kuthibitisha maneno
yaliyoandikwa kwenye ukurasa wake wa facebook, Kibatala alisema: “Ni kweli niliandika kwenye ukurasa wangu wa facebook na
ninaomba maneno hayo yabaki kama yalivyo, naona watu wengine wameanza kutafsiri
vinginevyo.”
Katika hukumu hizo, Majaji Projest
Rugazia na Penterine Kente waliwapa ushindi wabunge wawili wa Chadema, Susan
Kiwanga na Peter Liajualikali baada ya kukosekana ushahidi wa kutengua matokeo
hayo.
Juhudi za kumtafuta Mbilinyi
kuzungumzia hatua iliyochukuliwa dhidi yake hazikuzaa matunda kutokana na simu
zake zilizopigwa mara nyingi kutokuwa hewani.
No comments:
Post a Comment