
MKURUGENZI Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS), Rashid Othman amestaafu rasmi wadhifa huo, huku akitajwa kuwa miongoni mwa viongozi waliofanya kazi nzuri wakiongoza taasisi hiyo nyeti.
Habari za uhakika kutoka ndani ya
serikali, zilizopatikana jijini Dar es Salaam jana, zilisema kuwa Othman
alistaafu rasmi wadhifa huo Agosti 19, mwaka huu akiwa ameiongoza taasisi hiyo
tangu Agosti 20, 2006 ikiwa ni takribani miaka 10.
Kiongozi huyo aliteuliwa na Rais
mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete kuwa Mkurugenzi Mkuu ili kuziba nafasi
iliyoachwa na aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa wakati huo, Cornel Apson Mwang’onda.
Aliapishwa Ikulu Dar es Salaam
Agosti 21, 2006. Kabla ya uteuzi wake, Othman alikuwa Mkuu wa Utawala na
Utumishi wa Idara hiyo ya Usalama wa Taifa na kufanya kazi nzuri, iliyochangia
kumwezesha kuteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu.
Awali, Othman alitakiwa kustaafu
mwaka 2013 kwa mujibu wa sheria, lakini aliendelea kuongezewa mkataba wa mwaka
mmoja mmoja hadi alipokubaliwa kustaafu rasmi Ijumaa iliyopita.

No comments:
Post a Comment