
Mkutano Mkuu Maalum wa Chama Cha
Wananchi (CUF), uliofanyika jana jijini Dar es Salaam ukilenga kuwachagua
Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho ulivunjika baada ya wajumbe
kuanza kurushiana viti na matusi baada ya kupishana katika hoja ya kumtosa
aliyekuwa Mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba.
Profesa Lipumba alijiuzulu nafasi
yake kabla ya kampeni za uchaguzi Mkuu mwaka jana akieleza kuwa roho inamsuta
kumnadi mgombea urais aliyeungwa mkono na vyama vya Ukawa. Lakini mwaka huu
alirejea na kuandika barua akiomba kurejea kwenye nafasi yake hali iliyozua
sintofahamu.
Taarifa kutoka ndani ya Mkutano huo
zimeeleza kuwa wajumbe 832 walihudhuria lakini hoja ya kumjadili Profesa
Lipumba ilipofikiwa, baadhi ya wajumbe ambao wanamuunga Mwenyekiti huyo wa
zamani walizua vurugu wakipinga utaratibu uliotumika.
Baadhi ya wajumbe hao waliwaambia
waandishi wa habari kuwa viongozi waliopo madarakani walifanya ubabe kwa
kulazimisha kura ya kukubali au kukataa ombi la Lipumba ipigwe kwa uwazi na sio
siri kama Katiba inavyoeleza.
“Haki
haikutendeka, ni ubabe. Wala mkutano haikuzingatia kutimia kwa akidi.
Tulilazimishwa kupiga kura kwa kunyoosha mikono wakati mazingira yaliyopo na
usahihi, kura ni siri,” mmoja wa wajumbe hao alikaririwa.
Baada ya kupiga kura za wazi,
Lipumba alipata kura 14 kati ya kura 832 hivyo kuonekana kukataliwa kwa
kishindo, lakini vurugu zilizuka ghafla kutokana na maamuzi hayo na mkutano
ukashindwa kufanikisha zoezi zima la kuwapata viongozi hao wapya.
Katika hatua nyingine, Juma Haji
Duni alijiengeu katika kinyang’anyiro cha uchaguzi huo, baada ya baadhi ya
wajumbe kusisitiza kuwa katiba inamtaka mtu aliyejiuzulu na kuhamia chama
kingine kusubiri miaka miwili ili agombee nafasi ya uongozi ndani ya chama pale
atakaporejea.
Mkurugenzi wa Uchaguzi na Mipango
wa CUF, Shaweji Mketo, alisema kuwa Duni alijiondoa kutokana na maadui wa Ukawa
kutaka kukihujumu chama hicho.
Mkutano huo umeahirishwa hadi
utakapotangazwa tena.

No comments:
Post a Comment