
MSAJILI wa Vyama vya Siasa, Jaji
Francis Mutungi, ameitisha Baraza la Vyama vya Siasa ili kunusuru mvutano
uliojitokeza kati ya Jeshi la Polisi na Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema).
Jaji Mtungi amevitaka vyama vya
siasa vilivyotangaza kufanya maandamano na mikutano isiyo na tija nchi nzima
kuacha, badala yake warudi kwenye meza ya mazungumzo ili kuondoa tofauti
zinazojitokeza.
Kauli ya Jaji Mutungi imekuja baada
ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) nao kutangaza maandamano ya
amani kwa ajili ya kupongeza utendaji kazi wa Rais Dk. John Magufuli, huku
Chadema kikiitisha maandamano na mikutano isiyo na kikomo nchi nzima, ambayo
imepewa jina la Operesheni Ukuta.
Akizungumza na waandishi wa habari
Dar es Salaam jana, Jaji Mutungi alisema kufanyika kwa maandamano na mikutano
hiyo, hakuwezi kuondoa changamoto za kisiasa zilizopo, hivyo basi wanapaswa
kukaa kwenye meza moja kwa ajili ya kujadili tofauti zilizopo na kuzipatia
ufumbuzi.
“Ninawaomba wale wote wenye lengo
la kuitisha maandamano na mikutano ya kisiasa kuacha kwa sababu haiwezi
kusaidia kuondoa changamoto zilizopo, bali tunapaswa kukaa kwenye meza moja ya
mazungumzo ili tuweze kujadili tofauti hizo na kuzipatia majibu,” alisema Jaji
Mutungi.
Aliongeza kuwa licha ya kuwapo kwa
jitihada za viongozi mbalimbali kujadili suala hilo, lakini vyama hivyo
vimeonekana bado vikiendelea na misimamo yao ya kuitisha mikutano na maandamano
yasiyo na kikomo, jambo ambao linaweza kuleta hofu kwa wananchi.
Jaji Mutungi alisema katika kipindi
hiki ambacho wananchi wametulia, hakuna haja ya kuwatia hofu au wasiwasi ili
ionekane kuwa nchi ina ombwe kubwa la uongozi, jambo ambalo linaweza kurudisha
nyuma juhudi za kuleta maendeleo.
Alisema kutokana na hali hiyo,
wananchi wanapaswa kuheshimu utawala bora na kuacha kujadili mambo ambayo
yanaweza kuvuruga amani, badala yake wanapaswa kuangalia mustakabali wa taifa
kwa kufanya kazi na kuleta maendeleo.
“Wananchi wanapaswa kuondoa hofu kuhusiana
na migongano ya kisiasa inayojitokeza, kwa sababu hakuna ombwe la uongozi,
badala yake wanapaswa kufanya kazi kwa masilahi ya taifa ili waweze kuleta
maendeleo,” alisema.
Aliongeza kuwa kutokana na hali
hiyo, ameamua kuitisha mkutano wa Baraza la Vyama vya Siasa ambalo
linashirikisha vyama 22, vikiwamo CCM na Chadema wajadili mambo mbalimbali
ikiwamo migongano ya kisiasa, ili waweze kuendesha shughuli zao kistaarabu.
Alisema mkutano huo utafanyika
Agosti 29 na 30 mwaka huu ukishirikisha wadau mbalimbali.
Jaji Mutungi alisema kutokana na
hali hiyo, Agosti 26 kutakuwa na kikao cha kuratibu mkutano huo ambao anaamini
ni muhimu kwa ajili ya kuleta maridhiano baada ya tofauti za kisiasa
zilizojitokeza.
“Baraza hili ni forum muhimu ya
upatikanaji wa maridhiano ya kisiasa kama kuna tofauti zilizojitokeza, kuliko
kuitisha mikutano na maandamano yasiyo na tija ambayo yanaweza kusababisha
wananchi kupata hofu,” alisema.
Alisema hakuna jambo lenye ugumu
katika suala hilo, kwa sababu migongano iliyopo inajadilika ikiwa ni pamoja na
kupitia baadhi ya vifungu vya kisheria kwa ajili ya kufatuta mwafaka.
Akizungumzia suala la Chama cha
Wananchi (CUF), Jaji Mutungi alisema migongano iliyopo kwenye chama hicho
anaijua, lakini kwa sasa hawezi kuzungumzia lolote kwa sababu mkutano ujao
utashirikisha vyama vyote kikiwamo CUF.
“Mimi ni mlezi wa vyama vya siasa…
CUF ni miongoni mwa watoto wangu, najua udhaifu wa vyama vyote kikiwamo CUF
hadi ubora wao, hata migongano iliyojitokeza ndani ya chama hicho naijua,
lakini kwa sasa nashindwa kuongea lolote kwa sababu tuna mkutano wa Baraza la
Vyama vya Siasa ambalo litajadili mambo mbalimbali, ikiwamo suala la mgogoro wa
CUF,” alisema Jaji Mutungi.
Kutokana na hali hiyo, aliwataka
wanachama wa chama hicho kuondoa hofu kwa sababu suala hilo litapatiwa ufumbuzi
kwa kuondoa tofauti zilizopo.
Jaji Mutungi aliyesema hayo huku
wafuasi wa aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba,
wakidai kwenda katika ofisi yake kumweleza mambo mbalimbali, ikiwamo ya
ukiukwaji wa taratibu za kisheria na kumwondoa kiongozi huyo kwenye nafasi yake
uliofanywa na wafuasi wa Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad.
Katika hatua nyingine, Chadema
kimesema kimesikia wito wa Jaji Mutungi wa kuitisha mazungumzo ambayo iwapo
yatatawaliwa na nia njema na dhamira safi ya kuheshimu Katiba ya nchi, yanaweza
kuwa na manufaa kwa Watanzania wote.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya
habari Dar es Salaam jana na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa
chama hicho, Tumaini Makene, ilisema hatua hiyo inaweza kuleta manufaa
kama Jaji Mutungu hataegemea upande wa Serikali.
“Wakati Msajili wa Vyama akitoa
kauli ya kuzuia kile anachokiita ‘kutunishiana misuli’, Jeshi la Polisi katika
maeneo mbalimbali limeingilia vikao vya ndani vya chama na kuzuia visiendelee.
Hiyo yote ni kinyume na sheria, taratibu na mamlaka yao.
“Mbali na kuzuia vikao vya ndani,
Jeshi la Polisi linashikilia watu mbalimbali, wakiwamo wafuasi, mashabiki,
wanachama, viongozi wetu kwa kushiriki vikao hivyo, wakitekeleza wajibu
na haki zao za kikatiba na kisheria.
“Wakati tunasubiri meza ya
mazungumzo kupitia Baraza la Vyama, tunapenda kusisitiza kuwa Chadema itasimama
imara kuhakikisha misingi ya demokrasia na utawala unaozingatia Katiba na
sheria unafuatwa,” ilisema taarifa hiyo.

No comments:
Post a Comment