
RAIS John Magufuli ametoa ubani wa
Sh milioni 10 kwa familia za askari wanne waliouawa katika shambulio la
ujambazi Mbande wilayani Temeke mkoani Dar es Salaaam, huku akiwataka askari
kutokuvunjika moyo katika utendaji wao wa kazi kutokana na mauaji ya wenzao,
bali walitumie kama kigezo cha kufanya kazi kwa bidii.
Aidha, Rais Magufuli amemtumia
salamu za rambirambi Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali Ernest Mangu na
wanafamilia wa askari wote waliopoteza maisha.
Askari watatu kati ya wanne
waliofariki katika shambulio hilo la Jumanne usiku katika eneo la benki ya CRDB
Mbande, Dar es Salaam ambalo watu wenye silaha waliwavamia wakiwa kazini na
kuwaua na kupora bunduki mbili aina ya SMG na risasi 60, waliagwa jana katika
Viwanja vya Polisi Barabara ya Kilwa.
Akizungumza wakati wa kuaga miili
hiyo katika shughuli iliyoongozwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu
Nchemba, IGP Mangu alisema baada ya tukio hilo kutokea, aliwasiliana na Rais
Magufuli ambaye alionesha kusikitishwa sana na tukio hilo na kumpa pole yeye,
askari pamoja na familia za marehemu.
Miili ya askari walioagwa jana ni
Koplo Yahaya Malima aliyesafirishwa kwenda kuzikwa kijiji cha Kibuta, wilaya ya
Kisarawe mkoani Pwani, Tito Mapunda aliyesafirishwa kwenda kijiji cha Migoli,
wilaya ya Iringa Vijijini mkoani Iringa na Gaston Lupanga aliyesafirishwa
kwenda mjini Songea mkoani Ruvuma kwa maziko.
Askari mwingine Koplo Khatib Ame
Pandu alisafirishwa Jumatano jioni kwenda kwao Zanzibar ambako maziko
yalifanyika siku hiyo hiyo usiku.
Viongozi mbalimbali wa serikali
walipata fursa ya kutoa salamu za rambirambi katika msiba huo, na Mkuu wa Mkoa
wa Dar es Salaam, Paul Makonda aliamuru wale wote waliofanya uhalifu huo pamoja
na wale wanaofanya vitendo vya uhalifu jijini Dar es Salaam kushughulikiwa
ipasavyo.
“Katika hili ninaomba wale wa haki
za binadamu wanisamehe, kitendo hiki si cha kuvumilika hata kidogo kwa kuona
wale ambao wamekula kiapo kutulinda sisi, leo sisi tunakwenda kuwaua wao halafu
tunyamaze, mimi nasema hapa hadharani …Afande Sirro twanga tu yeyote
mtakayekutana naye msituni,” alisema Makonda.
Makonda alisema kazi ya amani ya
vyombo vya ulinzi ni kubwa hivyo ipo haja ya kuangaliwa upya kwa taratibu na
sheria kuona ni namna gani askari kama hao wanaopoteza maisha wakiwa bado
vijana wadogo kuwajengea hata nyumba ili kuwapa faraja wale wanaowaacha nyuma
yao.
Naye Kamanda wa Polisi Kanda
Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi Simon Sirro alisema kitendo
walichofanya wahalifu hao kuua askari ni sawa na kuwasha moto hivyo na wao
watajibu mapigo na kuhakikisha wahalifu hao wanapatikana.
“Wameuwasha moto na sisi tutauwasha
moto kwelikweli na katika hili tutaomba watu wa Tume za Haki za Binadamu
kutosimama upande wowote,” alisema Sirro.
Aidha, Waziri Mwigulu aliagiza
Jeshi la Polisi kuendelea bila kukoma kuwasaka majambazi na wahalifu wote na
kuhakikisha wanakamata waliofanya tukio hilo.
Mwigulu pia ameagiza viongozi wa
Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wizara yake kuangalia upya sheria na kuona
namna bora ya kuwasaidia askari kuwa na bima za maisha, huku akiwataka
kuhakikisha wanaharakisha mafao kwa familia za marehemu yanaandaliwa mapema.
“Mara nyingi kumekuwa na tabia ya
usumbufu kwa ndugu na jamaa za wafiwa kusumbuliwa na maandalizi ya mirathi
kuchukua muda mrefu na wakati mwingine tukio kama hili tumeshuhudia wote
lilivyotokea na askari wetu kufa wakiwa kazini lakini bado itaundwa tume
kuchunguza ili mafao yalipwe kwa wafiwa,” alisema Mwigulu.
Naye Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
George Masaju alisema kitendo cha kushambulia askari na kuwaua ni kuichokoza
mamlaka ya nchi na kulaani wote walioshabikia mauaji hayo kwa namna yeyote ile.
“Kitendo hiki si cha kushabikia na
tuache kabisa kushabikia vitendo vya uvunjifu wa sheria, lakini pia tutambue
kuwa sheria au Katiba ya Nchi haina mjadala,” alieleza Masaju.
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za
Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Bahame Nyanduga alilaani na kupinga mauaji ya
kikatili na kusema kuwa ni kinyume cha haki za binadamu na haki ya kuishi ya
kila mtu ipo ndani ya Katiba.
Mbali na Mwigulu, viongozi wengine
wa serikali waliotoa heshima za mwisho kwa miili ya marehemu ni Waziri wa Katiba
na Sheria, Dk Harison Mwakyembe, Masaju, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya
Nchi, Hamad Yussuf Masauni na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi,
Meja Jenerali Projest Rwegasira.
Pia IGP Mangu, Makonda, Mkuu wa
Wilaya ya Temeke, Felix Lyaniva, Meya wa Manispaa ya Temeke, Abdallah
Chaurembo, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Biswalo Mganga, Mkuu wa Makosa ya
Jinai, DCI, Diwani Athuman pamoja na makamishna mbalimbali wa Polisi, mahakimu
na wanasheria.
Katika hatua nyingine, mmoja wa
majeruhi katika tukio hilo, Said Ally (36) aliyelazwa katika Hospitali ya
Temeke, amefanyiwa upasuaji na kutolewa risasi aliyopigwa.
Ally ambaye ni mfanyabiashara
katika eneo la Mbande Magengeni karibu na benki ya CRDB ambako tukio hilo
lilitokea, alijeruhiwa kwa risasi hiyo wakati alipotoka nje ya duka lake
kuangalia kuna nini baada ya kusikia milio ya risasi.
Akizungumzia hali ya Ally, Ofisa
Habari wa Manispaa ya Temeke, Joyce Msumba alisema kwa mujibu wa taarifa
alizopewa na madaktari ni kwamba majeruhi huyo alifanyiwa upasuaji huo
jana.
“Taarifa nilizopewa ni kwamba
amefanyiwa upasuaji leo (jana) na ametolewa risasi ambayo ilikuwa mguuni kwake
pamoja na ganda la risasi, lakini anaendelea vizuri,” alisema
Msumba.
Majeruhi mwingine ni Azizi Ally
aliyekuwa akiuza chipsi katika mgahawa jirani na benki hiyo, alijeruhiwa na
risasi mkono wake wa kushoto wakati akikimbia kuokoa uhai wake.
Azizi ambaye alishonwa nyuzi sita
katika mkono huo, alisema anaendelea vizuri kwa kuwa alipata matibabu muda
mfupi baada ya tukio hilo na aliruhusiwa kurejea nyumbani.

No comments:
Post a Comment