Spika wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Job Ndugai, amekiri bunge hilo kusambaratika na kuwa
vipandevipande kutokana na vurugu za mara kwa mara zilizopelekea wabunge wa
upinzani kususia vikao hivyo anawaalika wabunge hao kwenye mazungumzo.
Ndugai, ambaye kipindi kirefu cha
Bunge la Bajeti lililomalizika hivi karibuni, alikuwa India kwa matibabu,
aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza kwenye kipindi cha Funguka
kinachorushwa na televisheni ya Azam.
Ndugai alisema ili bunge lifanye
kazi yake yake, linahitaji kuishinda changamoto iliyopo ya bunge kutokuwa kitu
kimoja, huku akielezea wazi kuwa chanzo kikuu kinachosababisha bunge hilo
kusambaratika ni pamoja na "u-vyama" kuzidi na wabunge kutojali
maslahi ya taifa.
Sababu nyingine aliyoitaja Ndugai,
ni ugeni wa wabunge ambapo kila unapofanyika uchaguzi sehemu kubwa ya wabunge
huwa ni wageni hivyo wengi wao wanakuwa hawajaelewa kanuni na tamaduni za
kibunge.
Alisema yanayotokea sasa kwa kiasi
kikubwa siyo mageni, yalikuwepo tangu wakati wa bunge la 10.
"Hali hii imeanza zamani
kidogo tangu enzi za spika Makinda, wabunge walikuwa wakitoka nje, wakigomea
vikao, wakiadhibiwa n.k. Ugumu ambao tunaupata ni kwamba kila baada ya uchaguzi
wanakuja wabunge wengi wageni ambao hawajui mambo mengi na mfano ni bunge hili
ambapo karibu 70% ya wabunge ni wapya" Alieleza Ndugai na kuongeza
kuwa hata suala la kumsusia Rais anapokwenda kuhutubia bungeni, limewahi
kutokea katika bunge lililopita.
Pamoja na hayo, Spika Ndugai
alisema kuwa hakuna kanuni inayomzuia mbunge kutoka nje ya bunge kwa kuwa ni
haki yake
"Hakuna kanuni inayomkataza
mbunge kutoka nje, ni sehemu ya demokrasia yao, lakini hii ya sasa imezidi, ni
jambo lisilopendeza... maana watanzania wamewatuma kwenda kuwakilisha hoja zao,
wanapotoka inakuwa haipendezi".
Aliwasihi wabunge wa Upinzani kurudi
bungeni na kueleza mambo yaliyowaudhi ili wakae wajadili na watafute ufumbuzi
badala ya kuendelea kususia.
Alisema "Wabunge
kutoka nje ni jambo ambalo halipendezi hata kidogo, nisingependa niendelee
kuliona.
"Nawaomba katika bunge lijalo
kama wanahisi tunakosea watueleze, na sisi tuwaeleze wanakosea wapi ili twende
sawa"
Kuhusu malalamiko ya wapinzani
dhidi ya Naibu Spika, alikiri kupokea malalamiko hayo kupitia kwa mbunge james
Ole Millya, na yeye aliyawasilisha kwenye kamati husika lakini hoja zote ambazo
walikuwa wakizilalamikia zilizonekana hazina uthibitisho, hivyo maamuzi ni
kwamba Naibu Spika Dkt Tulia Ackson hana hatia yoyote.
Kuhusu hoja ya Naibu Spika
kuendelea kukalia kiti kwa muda wote Ndugai anasema " Uongozi
ndiyo unapanga nani akae pale, sioni tatizo la mtu kukaa kwenye kiti kwa muda
mrefu, lakini kama mtu anakosea, zipo fursa za kupeleka jambo kwenye kamati
badala kulalamika bila kufuata kanuni"
Alisema haoni tatizo la Naibu Spika
na hajui ni mambo gani amewaudhi ila anadhani kinachowasumbua wapinzani ni
hisia za jinsi Naibu Spika alivyopatikana
"Wabunge wa upinzani wanapitia
changamoto nyingi kabla ya kuingia Bungeni, wengi wao wanahangaika sana kupata
ubunge hadi kufikia hatua ya kulala sana selo (polisi) kwaiyo namna ya 'kudeal'
nao inahitaji uvumilivu kidogo. Naibu Spika siyo mbunge wa jimbo, na wao
wamezoea mbunge wa jimbo ambaye anafanana nao, Naibu Spika ni mbunge wa uteuzi
kwahiyo wanahisi anafanya kazi kwa kufuata maelekezo kutoka nje ya bunge au
anatumikia mabwana wawili jambo ambalo siyo kweli. Pia adhabu zilizokuwa
zinatolewa zinawafanya wahisi wanaonewa kila wakati"
Pia Spika alikemea tabia ya baadhi
ya wabunge wa CCM kutumia muda mwingi bungeni kurusha vijembe kwa wabunge wa
upinzani
"Kwa wabunge wa chama tawala siyo
jambo zuri kurusha vijembe, tukienda bungeni nitakaa nao, na nitawaeleza kuwa
siyo jambo jema kuwa na bunge la vijembe, nawaasa tubadilike, tuheshimiane ...
matusi kelele vijembe kanuni haziruhusu na haipendezi"
Kuhusu mwenendo wa baadhi ya
wabunge kutoheshimu kanuni, Ndugai alisema "Kanuni zimetungwa kwa
watu wazima, lakini tatizo wabunge wanaokuja sasa hivi wengi ni vijana, na wako
chini ya kiwango cha kanuni. Bado sijajua nini cha kufanya ili hali hii
isiendelee, kwenye bunge la katiba angalau kulikuwa na kitu kinaitwa kamati ya
maridhiano, nafikiri inabidi tuige kitu hicho tupate watu hata wastaafu
watakaokuwa wanakaa kuyaweka mambo haya sawa"
Kuhusu sakata la Lugumi, Ndugai
alisema kuwa kamati ndogo iliyoundwa kufuatilia suala hilo itatoa taarifa yake
katika mkutano ujao wa bunge.
Kuhusu uamuzi wa serikali kuzuia
Bunge LIVE, Ndugai alisema uamuzi huo ni mzuri na anauunga mkono kwa kuwa
unasaidia kupunguza vurugu kwa wabunge.
Kuhusu suala la posho za wabunge
Naibu Spika alisema kuwa posho za wabunge wanazolipwa sasa, ni za kawaida na
siyo kubwa kama watu wanavyodhani huku akiunga mkono uamuzi wa wabunge kukatwa
kodi kwenye kiinua mgongo.
No comments:
Post a Comment