RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein, ametoa taarifa rasmi ya
Serikali kuhusu kifo cha Rais Mstaafu wa Zanzibar wa Awamu ya Pili, Mheshimiwa
Alhaj Aboud Jumbe Mwinyi.
Katika taarifa hiyo aliyoitoa jana
kupitia vyombo vya habari, Alhaj Dk. Shein kwa masikitiko makubwa aliwaarifu
wananchi kuwa jana tarehe 14 Agosti 2016, Mzee Alhaj Aboud Jumbe Mwinyi
amefariki dunia, msiba ambao umetokea nyumbani kwake Mji Mwema, Dar es Salaam.
Alhaj Dk. Shein alieleza kuwa
Marehemu Mzee Aboud Jumbe ni Rais Mstaafu wa Zanzibar wa Awamu ya Pili, ambaye
vile vile alikuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo
Marehemu Mzee Aboud Jumbe amefariki dunia baada ya kuugua kwa muda mrefu
kutokana na umri wake.
Kwa taarifa ya Alhaj Dk. Shein,
maziko ya marehemu yatafanyika leo tarehe 15 Agosti 2016 saa 7.00 mchana ambapo
maiti yake itasaliwa katika Masjid Mshawar, Mwembeshauri na kuzikwa nyumbani
kwake Migombani.
Aidha, Alhaj Dk. Shein alieleza
kuwa kufuatia mchango na juhudi kubwa ambazo Marehemu Mheshimiwa Aboud Jumbe
Mwinyi alizichukua katika uhai wake kwa kuitumikia, kuiongoza na kuijenga
Zanzibar pamoja na nafasi yake katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Nchi yetu imekabiliwa na msiba
mkubwa kwa kifo cha kiongozi huyu mahiri”alieleza Alhaj Dk. Shein katika
taarifa hiyo.
Kutokana na msiba huo mkubwa Alhaj
Dk. Shein alitangaza rasmi siku saba za maombolezo, kuanzia leo tarehe 15
Agosti 2016 ambapo katika kipindi hicho chote bendera zote zitapepea nusu
mlingoti.
Pamoja na hayo, Alhaj Dk. Shein
alieleza kuwa utaratibu wa maziko utafuata wasia ambao mwenyewe marehemu
aliutoa wakati wa uhai wake.
“Tunaungana na Wanafamilia wote
katika kipindi hiki kigumu cha msiba. Naomba kutumia nafasi hii kutoa mkono wa
pole kwa wafiwa wote. Tunamuomba Mwenyezi Mungu amjaalie kauli thabit marehemu
mzee wetu na amlaze pahala pema peponi, Amin. Inalillahi wainnailaihi rajiun”Alieleza Alhaj
Dk. Shein katika Taarifa hiyo.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422
Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail:
rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment