POLISI mkoani Kigoma imewatia
mbaroni watu watano akiwemo askari mmoja wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa
Tanzania (JWTZ) kwa tuhuma za kutengeneza vyeti bandia vya kitaaluma, miongoni
mwake vikiwemo 90 vya uuguzi, ambavyo vilikutwa vikisubiri kugawiwa kwa
wahusika.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Ferdinand Mtui alisema kuwa pamoja na vyeti hivyo vya uuguzi vilivyokamatwa, pia katika operesheni hiyo walikamata vyeti 37 vya wataalamu wa maabara na vyeti tisa vya ufamasia.
Alisema kuwa katika operesheni hiyo
iliyofanywa kwa pamoja na maofisa kutoka Baraza la Wafamasia nchini, walikamata
jumla ya vyeti 936 vikiwa kwenye hatua ya ukamilishaji vikiwa bado
havijaandikwa majina, miongoni mwake vikiwemo vyeti 667 vya wauguzi wasaidizi,
vyeti 126 vya wataalam wa maabara, cheti kimoja cha mafunzo ya afya ya jamii na
vyeti viwili vya utoaji huduma ya kwanza.
Katika kuhakikisha wanakuwa na
uthibitisho wa tuhuma hizo, Kamanda Mtui alisema kuwa pia wamekamata mihuri 25
ya taasisi mbalimbali ikiwemo nyundo mbili, ambazo hutumika kutengenezea mihuri
mbalimbali ya moto.
Aliwataja watu waliokamatwa katika
operesheni hiyo ambayo inahusisha mtandao wa watu mbalimbali kuwa ni askari wa
JWTZ, Mgeni Nyamubozi ambaye ni mume wa mmiliki wa Duka la Vifaa vya Ofisi la
Upendo, lililopo Mwanga mjini Kigoma, ambalo linatuhumiwa kuhusika na
utengenezaji wa vyeti hivyo.
Katika duka hilo, Kamanda huyo wa
polisi alisema polisi walikamata kompyuta mpakato moja, ikiwa na nakala za
vyeti mbalimbali za vyuo na idara za serikali.
Mwingine aliyekamatwa ni Dickson
Mshahili, muuguzi katika Hospitali ya Mkoa Kigoma ambaye katika upekuzi
nyumbani kwake, alikutwa na nyaraka mbalimbali ikiwemo madaftari 12 yakiwa na
kumbukumbu za vyeti anavyotengeneza na mihuri ya waganga wakuu wa mikoa ya
Kigoma, Kagera, Mwanza, Singida na Tabora.
Sambamba nao alikamatwa Zawadi
James, muuguzi wa Kituo cha Afya Ujiji ambaye baada ya kupekuliwa nyumbani
kwake, alikutwa na vyeti vitatu na kabuleta ya pikipiki ambayo hutumika
kutengeneza mihuri ya moto.
Wengine waliokamatwa ni Johnson
Nyabuzoka, mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Mlole ya mjini Kigoma, ambaye ni
mtaalam wa kompyuta aliyekuwa akitumika kufanya kazi hiyo; na Stephano Erasto
ambaye alikamatwa katika siku yake ya kwanza tangu ajiunge na duka hilo kwa
ajili ya kusaidia kazi.
No comments:
Post a Comment