WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa
siku mbili kwa Mkuu wa Idara ya Ardhi na Miundombinu wa mkoa wa Rukwa pamoja na
Ofisa Ardhi wa Manispaa ya Sumbawanga kutatua matatizo ya ardhi yanayowakabili
wakazi wa Manispaa hiyo.
“Ijumaa kuanzia saa 3.00 asubuhi
wenye kero za ardhi wote waende kwenye ukumbi wa Manispaa mkuu wa idara atakuwa
na watumishi wote na hapa mtasikilizwa kero zenu na kupatiwa ufumbuzi. Nasiku
hiyo hakuna kazi nyingine ni kusikiliza wananchi tu,” alisema.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana
jioni (Jumatano, Agosti 24, 2016) wakati akizungumza na maelfu ya wakazi Mji wa
Sumbawanga waliojitokeza katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kiwanja
cha Mandela katika jimbo la Sumbawanga mjini ambapo aliwasisitiza watendaji hao
kuwasikiliza wananchi na kutatua kero zao.
Alisema tangu alivyoanza ziara yake
katika mikoa ya Rukwa na Katavi kila eneo alilopita amekutana na wananchi
wakiwa na mabango yanaeleza changamoto na hii inatokana na viongozi wa mikoa
hiyo kushindwa kutenga siku maalumu kwa ajili ya kusikiliza kero hizo.
Waziri Mkuu alibainisha kwamba
baadhi ya mikoa na halmashauri mbalimbali nchini zimeshaanza utaratibu huo wa
kutenga siku maalumu katika wiki na kusikiliza matatizo yanayowakabili wananchi
jambo ambalo limeanza kuonesha mafanikio ya utatuzi wa kero hizo.
Awali akizungumza katika mkutano
huo mbunge wa jimbo la Sumbawanga Mjini Aeshi Hilaly alisema wakazi wa Manispaa
ya Sumbawanga wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya migogoro mikubwa
ya ardhi, hivyo alimuomba Waziri Mkuu kuwasaidia katika kuipatia ufumbuzi.
Mbunge huyo alisema migogoro hiyo
ambayo imedumu kwa muda mrefu imewasababishia usumbufu mkubwa wakazi wa jimbo
hilo kukosa haki zao na muda mwingi wamekuwa wakiutumia kufuatilia hatma
ya ardhi yao bila ya mafanikio hivyo kurudi nyuma kimaendeleo.
Pia mbunge huyo alimuomba Waziri
Mkuu kuwaondolea zuio la kuuza mazao yao nje ya nchi kwa sababu kitendo hicho
kimesababisha kushuka bei ya mahindi na kusababisha hasara kubwa kwa wakulima
ambao wametumia gharama kubwa katika kuandaa mashamba.
Akizungumzia zuio hilo Waziri Mkuu
alisema lengo la Serikali kuzuia uuzwaji wa mazao nje ni kutaka kujiridhisha na
uwepo wa chakula cha kutosha nchini ili kuepuka kukumbwa na baa la njaa
na kisha kwenda kuomba msaada kwenye nchi tuliowauzia.
Kuhusu suala la soko la mahindi Waziri Mkuu alisema Wakala
wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) watanunua kwa bei ya soko na kwamba
wataruhusiwa kuuza nje ya nchi baada ya Serikali kujaza maghala yake huku
wataalam wakimalizia kufanya tathmini ya hali ya chakula nchini
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI
MKUU,

No comments:
Post a Comment