Waziri Kassim Majaliwa amesema
safari ya kuhamia Dodoma imeiva na amewataka watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu
wajipange kisaikolojia.
Ametoa kauli hiyo leo Agosti 18,
2016 alipokutana na kuzungumza na watumishi wa ofisi yake kutoka taasisi, idara
na vitengo mbalimbali waliopo Dar es Salaam.
Waziri Mkuu amewataka watumishi hao
watambue kuwa uamuzi wa Serikali kuhamia Dodoma ni utekelezaji wa Ilani ya
Chama cha Mapinduzi (CCM) ambao chimbuko lake ni agizo lililotolewa Oktoba
Mosi, 1973 kwenye Mkutano Mkuu wa 16 wa chama cha TANU.
“Tangu wakati huo kumekuwa na
juhudi mbalimbali zilizofanyika ili kuandaa miundombinu na hata awamu ya nne ilisimamia
kwa kiwango kikubwa uwekaji wa miundombinu hiyo,” amesema.
“Pia tukumbuke kauli ya Mheshimiwa
Rais aliyotoa kwenye hotuba yake ya Julai 23, 2016 alipochaguliwa kuwa
Mwenyekiti mpya wa CCM, na akairudia tena Julai 25, kwenye maadhimisho ya kumbukumbu
ya Mashujaa na mimi siku hiyo hiyo nikaweka msisitizo,” amesema.
“Napenda kuwatoa hofu, mambo
yanaenda vizuri ila mtambue kuwa safari imeiva sasa. Kikubwa ni kwamba
tutakwenda kwa awamu kama ambavyo imepangwa,” amesema.
Amewataka watumishi hao wazidishe
mshikamano miongoni mwao huku wakitambua kuwa wana dhamana ya kuwatumikia
Watanzania kwa uadilifu na uaminifu.
“Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu
tunapaswa tutambue dhamana tuliyonayo. Tufanye kazi kwa bidii. Tuhakikishe kila
kilichopangwa kinafanyika kwa ufanisi na kinafanikiwa,” amesema.
Julai 25 katika maadhimisho ya Siku
ya Mashujaa, Waziri Mkuu aliwataka mawaziri wote kuhamia Dodoma mara moja na
kusema kuwa yeye atakuwa wa kwanza ifikapo Septemba.

No comments:
Post a Comment