
Na: Lilian Lundo-Maelezo
Mwenyekiti wa Chama cha UDP John Cheyo amesema kuwa Mhe. Rais
Dkt. John Pombe Magufuli ni Rais aliyesubiriwa kwa muda mrefu tangu kuanza kwa
Uhuru.
Cheyo ameyasema hayo alipokuwa akielezea juu ya utendaji wa Rais
Magufuli tangu ameingia madarakani Novemba, 2015.
“Utendaji wa Rais Magufuli umewashtusha watu wengi kwani
hawakutegemea kwa muda mfupi aliokuwa madarakani kama angeweza kuchukua hatua
kubwa kama vile kupambana na mafisadi, jambo ambalo limekuwa likiongelewa na
viongozi waliopita lakini kulikuwa hakuna matunda ya moja kwa moja,” alifafanua Cheyo.
Ameendelea kwa kusema kuwa Rais Magufuli amekuwa na adhima ya
kupambana na Mafisadi na kutatua kero za Taifa tangu akiwa kwenye kampeni huku
akisimamia kauli mbiu ya Hapa Kazi Tu.
Vile vile Cheyo amesema kuwa kero ambazo amekuwa akizitatua Rais
Magufuli zikiwemo ufisadi, uchumi tegemezi, mapato madogo na ukosefu wa vifaa
mahospitalini ni kero ambazo zimekuwa zikipigiwa kelele na kambi ya upinzani
kwa muda mrefu.
Hivyo kuingia kwa Rais Magufuli madarakani kumeleta utatuzi
mkubwa kwa kero hizo ambazo zimekosa utatuzi kwa muda mrefu kutokana na
viongozi waliopita kutozichukulia uzito mfano Rais Magufuli alivyoweza kutatua
tatizo la vitanda hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa kipindi kifupi ambapo
hivi sasa hakuna mgonjwa anayelala nchini katika hospitali hiyo.
Akielezea suala la ufisadi nchini, Cheyo amesema kuwa ufisadi ni
ugonjwa wa muda mrefu ambao umepoteza fedha nyingi za nchi kutokana na mikataba
mibovu iliyokuwa ikisainiwa na viongozi wa juu.
Aidha amempongeza Mhe. Rais kwa kuanzisha Mahakama ya Mafisadi
na kuona tatizo hilo lishughulikiwe kisheria na kwa njia maalum ili kukomesha
ufisadi nchini.
Cheyo amewataka watanzania kugeuza mawazo yao na kuchukia rushwa
kwa kukataa kupokea na kutoa rushwa kwani rushwa ni adui wa haki na inarudisha
nyuma maendeleo ya nchi.

No comments:
Post a Comment