
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya siasa
nchini imemuandikia barua Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif
Sharif Hamad kufuatia mvutano wa kusimamishwa uanachama aliyekuwa Mwenyekiti wa
chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya
Profesa Lipumba kumuandikia barua Msajili wa vyama vya siasa nchini, Jaji
Francis Mutungi akilalamikia kusimamishwa uanachama bila kufuata utaratibu huku
akitaka kurejeshwa kwenye nafasi yake ya uenyekiti.
Ofisi hiyo imeutaka uongozi wa CUF
kueleza kwa kina hatua ilizopitia hadi kufikia uamuzi huo kwa mujibu wa katiba
ya chama hicho, na kwamba iwasilishe barua hiyo kufikia kesho majira ya saa
9:30 alasiri.
Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano cha
Ofisi ya Msajili wa Vyama Vya Siasa, Monica Laurent amesema kuwa ofisi hiyo
ilipokea barua ya Profesa Lipumba Agosti 29 mwaka huu ikiwa na malalamiko na
kwamba wametaka uongozi wa CUF kutolea majibu.
“Tumeitaka CUF kutoa majibu kuhusu
malalamiko ya Profesa Lipumba, ndipo sisi tutakapotoa majibu,” amesema Monica.
Lipumba ambaye alijiuzulu nafasi
yake ya Uenyekiti mwaka jana akipinga uamuzi wa chama chake kumuunga mkono
Edward Lowassa kugombea urais, amerejea na kudai kutengua barua yake ya
kujiuzulu.
Baraza Kuu la CUF lililoketi visiwani
Zanzibar hivi karibuni lilimsimamisha uanachama Profesa Lipumba pamoja na
viongozi wengine 10 akiwemo Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya aliyekuwa Naibu
Katibu mkuu (Bara).
Hata hivyo, Profesa Lipumba
amepinga uamuzi huo akieleza kuwa kikao cha baraza hilo kililiwa batili.

No comments:
Post a Comment