
VIFAA vilivyokamatwa jana vya klabu
ya usiku ya Bilicanas na ofisi ya gazeti la Tanzania Daima, vyote
vinavyomilikiwa na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
Freeman Mbowe, vitapigwa mnada na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) siku 14
kuanzia jana, endapo atashindwa kulipa Sh. bilioni 1.2 za deni la pango la
miaka 20.
Mbowe alikuwa mpangaji katika jengo
la NHC lililopo makutano ya mitaa ya Mkwepu na Indira Gandhi, katikati ya jiji
la Dar es Salaam.
Vyombo hivyo vilikamatwa jana na
kampuni ya udalali ya Fosters Auctioneers and General Traders iliyopewa kazi ya
kuondoa vifaa hivyo baada ya Mbowe kushindwa kulipa deni hilo ndani ya miezi
miwili ya notisi ambayo shirika hilo lilikuwa limempatia.
Meneja wa Kitengo cha Kukusanya
Madeni kutoka NHC, Japhet Mwanasenga aliyekuwa akisimamia ukamataji wa vyombo
hivyo, alisema Mbowe ana muda wa wiki mbili kuanzia jana kulipa deni la Sh.
bilioni 1.172 vinginevyo vitapigwa mnada.
Vifaa vilivyokamatwa ni pamoja na
kompyuta, meza na viti.
Alisema taratibu zote zilifuatwa
kabla ya kumuondoa mteja wao, ikiwamo notisi na kwamba vifaa hivyo
vitashikiliwa kwa muda huo wa wiki mbili.
“Tunashikilia vyombo kwa muda wa
wiki mbili na iwapo atashindwa kulipa vitapigwa mnada na dalali, (mdaiwa)
akishindwa kulipa anapangishwa mwingine,” alisema.
Alisema shirika hilo linahitaji
fedha kwa ajili ya ujenzi na uendelezaji wa majengo yake hivyo mteja ambaye
anadaiwa ajiandae kuondolewa wakati wowote na kwamba zoezi la jana ni mwanzo
tu.
Baadhi ya watu wamelihusisha tukio
la kuondolewa Mbowe katika ofisi hizo na masuala ya kisiasa.
Lakini Mwanasenga alisema uamuzi wa
kumuondoa ofisi hizo hauna uhusiano na masuala ya kisiasa.
Alisema wapangaji wa jengo hilo
wapo wengi pamoja na wadaiwa na kwamba baada ya mchakato huo kuanza mdaiwa
yeyote atakayeshindwa kulipa kodi ataondolewa.
Akizungumza na waandishi wa habari
katikati ya wiki iliyopita, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemia Mchechu alisema
pamoja na Bilicanas, shirika linazidai taasisi za umma, binafsi na watu binafsi
jumla ya Sh. bilioni 15.
Notisi ya siku 60 ya kuondoka
Bilicanaa pamoja na majengo ya wadaiwa wengine ilishatolewa, Mchechu alisema.
Notisi hiyo ilikuwa inaisha juzi.
Alisema baada ya muda huo
kumalizika, utekelezaji wa kuondolewa katika majengo hayo utaanza ukiambatana
na uchukuaji wa hatua za kisheria.
Mchechu alisema mbali ya Bilicanas,
wadaiwa wengine ni Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi inayodaiwa Sh. bilioni
mbili, Benki ya Azania (Sh. milioni 161) na Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano
wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa (Sh. milioni 631).
Wadiawa wengine walitajwa kuwa ni
Wizara ya Afya na Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Sh. bilioni
1.3), Wizara ya Ujenzi (Sh. bilioni mbili), Tume ya Utumishi (Sh. milioni 109)
na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Sh. bilioni moja.
Mchechu alisema ukusanyaji wa
madeni hayo kwa nguvu ni mkakati wa shirika hilo kukusanya fedha ili kusaidia
ujenzi wa nyumba za watumishi wanaohamia Dodoma.
"Mwaka huu ujenzi unaanza
Dodoma," alisema Mchechu, hivyo "fedha tunazodai zitatusaidia
kukamilisha uwekezaji mjini humo."
Alisema kuwa fedha hizo zitatumika
kwa ujenzi wa nyumba za watumishi 300 hadi 500 mkoani Dodoma.
Alisema ujenzi huo unatarajia
kuanza mara moja na utachukua miezi 12.
Kwa mujibu wa Mchechu, Sh. bilioni
60 za ujenzi wa nyumba hizo zitatokana na fedha za ndani.
Alisema shirika hilo limenunua
ekari 240 eneo la Iyumbu, ekari saba Chamwino, nne Bahi na Chemba ekari nne pia
ikiwa ni kuunga mkono azma ya serikali ya awamu ya tano kuhamia Dodoma.
Alisema fedha nyingine zitapatikana
baada ya nyumba 97 za shirika hilo zilizopo Medeli mjini Dodoma kuuzwa.

No comments:
Post a Comment