
Rais wa Jamhuri ya Sudan Kusini
Mhe. Salva Kiir Mayardit amemtumia ujumbe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki akimuarifu kuwa hali ya usalama katika nchi hiyo imeanza kutengemaa.
Rais Salva Kiir Mayardit
amewasilisha ujumbe huo kupitia kwa Mjumbe wake Maalum Mhe. Aggrey Tisa Sabuni
ambaye pamoja na kuwasilisha ujumbe huo amesema Sudani Kusini imekamilisha
nyaraka za azimio la kuridia mkataba wa kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki
ambao umewasilishwa jana tarehe 05 Septemba, 2016 katika makao makuu ya Jumuiya
Jijini Arusha.
Mhe. Aggrey Tisa Sabuni amesema
Sudan Kusini ipo tayari kushirikiana na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki katika masuala mbalimbali yenye manufaa kwa wananchi ikiwemo biashara
na uwekezaji na kwamba ni matumaini yake kuwa itapata ushirikiano mzuri.
Kwa upande wake Rais Magufuli
ameelezea kufurahishwa kwake na taarifa za kutengemaa kwa hali ya amani nchini
humo na kwamba ni matarajio yake kuwa Sudan Kusini itajikita katika maendeleo
ya wananchi wananchi wake.
Katika hatua nyingine, Rais
Magufuli amepokea ujumbe kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Burundi Mhe. Pierre
Nkurunziza ulioletwa na Mjumbe Maalum wa Rais huyo Mhe. Aime Laurentine
Kanyana.
Katika ujumbe huo Rais Nkurunziza
amesema hali ya Burundi ni shwari na kwamba wananchi wa Burundi wanaendelea na
shughuli zao kama kawaida.
Kwa upande wake Rais Magufuli
amesema Tanzania yenye wakimbizi takribani 200,000 wa kutoka Burundi
inafurahishwa na taarifa za kuwepo hali ya amani nchini humo.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais,
IKULU
Dar es Salaam
06 Septemba, 2016

Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akipokea ujumbe maalum kutoka kwa
Rais wa Burudi uliowasilishwa kwake na Aime Laurentine Kanyana Waziri wa Mambo
ya Nje wa Burundi Ikulu jijini Dar es Salaam. Picha na IKULU

No comments:
Post a Comment