
UMOJA wa Vijana wa Chama Cha
Mapinduzi (UVCCM) umesema Rais John Magufuli, hana baya alilolitamka katika
mikutano yake ya Unguja na Pemba, bali amezika upotoshaji wa siasa uchwara,
kusafisha upepo mchafu na kufumba vinywa vya wanasiasa wakorofi na wazushi.
Pia umetoa mwito kwa Wazanzibari
kwa nguvu zote kupinga siasa chafu au zenye lengo la kuwagawa, kuwatenganisha
au kuwahasimisha badala yake watambue umuhimu wa kuendeleza umoja, amani na
maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka
Hamdu Shaka alisema hayo ofisini kwake Makao Makuu ya CCM, Dodoma, alipotakiwa
kueleza maoni yake kuhusu shutuma anazotupiwa Rais Magufuli ikidaiwa na baadhi
ya wanasiasa kwamba alilenga kuamsha joto la mtafaruku wa kisiasa visiwani
humo.
Shaka alisema hotuba ya Rais Dk
Magufuli imezima siasa za uzushi na dhidi ya viongozi wanaowadanganya wafuasi
wao kwamba utafanyika Uchaguzi Mkuu mwingine kabla ya mwaka 2020 na Rais Ali
Mohamed Shein ataondoka madarakani ili kumpisha Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif
Sharif Hamad.
Shaka alisema hotuba ya Rais
ilikuwa yenye mashiko na maudhui, makatazo, maonyo, maelezo na wosia
uliojiegemeza katika kudumisha amani nchini.
“Kuhubiri amani ni dhamana yake
kiutawala, kuwaonya wananchi wanaokata mikarafuu, kutoboa mitumbwi, kufyeka
mazao mashambani na wengine kukataa kuwauzia bidhaa wenzao halikuwa kosa na si
jambo baya kama inavyoelezwa na wazushi wa kisiasa,” alisema Shaka.
Aidha, alisema ikiwa kuna
mwanasiasa asiyemtii Rais aliye madarakani Zanzibar na hata kukataa hata mkono
wake, hakuna sababu kwa kiongozi huyo kutaka msaada kwenye serikali
asiyoitambua.
“Iweje baniani mbaya kiatu chake
dawa, unajigamba humtambui Rais aliyeshinda na kuunda serikali ila unadoea
fedha zinazokusanywa na serikali usioitambua ili usaidiwe na kulipwa
marupurupu. UVCCM inaunga mkono SMZ kumnyima stahili zote hadi atakaipomtambua
Rais,” alisema Shaka.
Kaimu Katibu Mkuu huyo alisema
wakati wa utawala wa Dk Salmin Amour Juma, Maalim Seif aliposema hamtambui kama
mshindi halali hakuwa akilipwa chochote, Rais mstaafu Amani Abeid Karume
hakumlipa kitu hadi alipojipeleka Ikulu Novemba 5, 2009 akatangaza kuitambua
serikali yake.
Alisema matamshi ya Dk Magufuli
katika hotuba zake zote, ameweka bayana kila kitu, amewakanya wanasiasa
wachochezi na hatarishi kwa amani, amewaonya viongozi katika serikali zote huku
akikataa uzembe, urasimu, ubadhirifu wa mali za umma na kusema wote wasiotosha,
wajipime iwapo bado wanafaa au la.

No comments:
Post a Comment