
Na Ismail Ngayonga - Maelezo.
SERIKALI inakusudia kuwapeleka
katika kambi za mafunzo ya Jeshi la Kuujenga Taifa (JKT) watoto wa
mitaani wenye umri wa zaidi ya miaka 18 ili wajifunze stadi za kazi na
shughuli za uzalishaji mali.
Hayo yamesemwa jana na Waziri wa
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu
wakati wa mahojiano maalum katika kipindi cha Tunatekeleza kinachoandaliwa na
Idara ya Habari (MAELEZO) na Televisheni ya Taifa (TBC1).
Waziri Ummy alisema hatua hiyo
inalenga kuliwezesha kundi hilo la vijana kujihusisha na shughuli za uzalishaji
mali badala ya kuzurura hovyo mitaani sambamba na kujihusisha na tabia na
vitendo vinavyokiuka maadili katika jamii.
Alisema tayari watendaji wa
Wizara yake kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Waziri Mkuu tayari wamekutana kujadiliana kuhusu
suala hilo ili kuangalia namna bora zaidi ya kusadia kundi hilo.
Alifafanua kuwa vituo vingi vya
kulelea watoto hao vimekuwa na watoto waliozidi umri wa miaka 18, ambapo kwa
mujibu wa sheria hawatakiwi kuwa katika vituo hivyo na kuongeza kuwa
ofisi yake itahakikisha zoezi la kuwapeleka katika mafunzo hayo linatekelezeka.
Katika hatua nyingine Waziri Ummy
alipiga marufuku tabia za baadhi ya watu, asasi na vikundi kuanzisha
vituo vya kulea watoto yatima pasipo kuwa na usajili kwani kufanya hivyo
ni kosa kisheria.
Kwa mujibu wa Waziri Ummy alisema
tayari ofisi yake imetoa maelekezo kwa Kamishina wa Ustawi wa jamii kufanya
tathimini na utafiti wa kina kuhusu vituo vya kulea watoto yatima, ambapo iwapo
kutabainika vituo vitakavyokosa sifa hatua za kisheria zitachuliwa kwa
wahusika.
Kuhusu chanjo, Waziri Ummy alisema
Serikali itaanza kutoa chanjo ya saratani ya shingo ya kizazi kwa watoto wenye
umri wa miaka 9-13 ili kukabiliana na changamoto ya maradhi hayo nchini.
Waziri Ummy aliwataka wazazi kutoa
ushirikiano pindi zoezi hilo litakapoanza kwa kuwa halitakuwa na madhara ya
kiafya kwa watoto wao.
Aidha, alisema Serikali
imekuwa ikipoteza kiasi kikubwa cha fedha kila mwaka kwa ajili ya matibabu ya
magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo saratani ya shingo ya kizazi kwa akina mama
ambayo inaambukizwa na virusi vinavyojulikana kwa jina la Human Papiloma Virus
(HPV).
“Tumeamua kuteua kundi la watoto wa
lika huo kwani wengi wao katika umri huo wanakuwa bado hawajaanza kujihusisha
na vitendo vya mapenzi” alisema Waziri Ummy.
Alisema katika bajeti ya mwaka
2016/17 Serikali imepanga kuipatia taasisi ya saratani ya ocean road
kiasi cha Tsh. Bilioni 3 kwa ajili ya ununuzi wa madawa, ikilinganishwa na
kiasi cha Tsh. Milioni 600 zilizokuwa zimetengwa katika bajeti ya mwaka
2015/16.
Akizungumzia changamoto
iliyojitokeza hivi karibuni ya ukosefu wa chanjo katika vituo vya huduma ya
hivi nchini, Waziri Ummy alisema suala hilo litakuwa historia hivi karibuni
kwani tayari Serikali imeagiza kutoka nje ya nchi baadhi ya chanjo hizo.
No comments:
Post a Comment