
Na Jacquiline Mrisho-Maelezo
SERIKALI kupitia Wizara ya Elimu,
Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi imewaasa vijana waliomaliza shule
kuacha kujibetweka bali watumie elimu waliyoipata kujitafutia ajira ili
kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira nchini.
Kauli hiyo imetolewa jana Jijini
Dar es Salaam na Kaimu Kamishna wa Elimu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi
Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Nicholaus Bureta wakati wa ufunguzi wa mkutano
wa vijana wa Afrika unaojadili changamoto zinazowakabili vijana katika nyanja
mbalimbali za maendeleo.
Bureta alisema kuwa Serikali
inatoa elimu bora ili kuhakikisha vijana wanapata uwezo na maarifa
yatakayowasaidia kujiajiri hata wasipopata nafasi za kuajiriwa katika taasisi
na ofisi za umma pamoja na kuitumia elimu hiyo katika kupambana na vitendo vya
rushwa.
“Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka
2014 inatutaka tuwe na watanzania walioelimika na wenye mtazamo chanya ambao
utahakikisha jamii yetu inabadilika kufikia uchumi wa kati hivyo vijana msikae
kusubiri ajira bali mjifunze jinsi ya kujiajiri kutokana na elimu mliyoipata
mashuleni”, alisema Bureta.
Kwa upande wake Afisa Habari wa
Umoja wa Mataifa (UN), Stellah Vuzo aliwapongeza vijana hao kuamua kukusanyika
kuchangia mawazo yao juu ya matatizo yanayowakabili kwani vijana wana nafasi
kubwa ya kuhakikisha malengo mbalimbali yanatekelezeka.
Aidha, aliongeza kuwa Umoja wa
Mataifa umemteua balozi kijana ambaye anashughulikia ajira za vijana hivyo
aliwaomba vijana walioshiriki katika mkutano huo kuyafikisha mawazo hayo kwa
balozi huyo ili yaweze kupatiwa ufumbuzi.
Naye Mkuu wa Utafiti kutoka Taasisi
ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (PCCB), Daniel Pundu alisema kuwa tatizo la
rushwa haliwezi kuisha endapo vijana hawatashirikishwa hivyo amewasisitiza
vijana kushirikiana na Serikali kuchukua hatua za kupambana na rushwa ili
kuhakikisha rushwa inaondoka.
“Tunajua kuwa vijana ndio nguvu
kazi ya Taifa na ndio sababu tunawasisitiza kupambana na rushwa, kwa kulitambua
hilo Serikali imeanzisha vilabu vya wapinga rushwa katika shule za sekondari na
vyuo vikuu vikiwa na lengo la kuhakikisha vijana wanahusika kwenye mapambano
hayo”, alisema Pundu.
No comments:
Post a Comment