
Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa
Tanzania limesikitishwa na taarifa iliyotolewa na gazeti la Tanzania Daima
toleo Nambari 4290 la tarehe 01 Septemba 2016, ikihusisha shughuli za Jeshi
hilo zinazoendelea katika maadhimisho ya miaka 52 ya kuzaliwa kwake na shughuli
za kisiasa.
Tunapenda kuwataarifu
wananchi kwamba kazi ya Jeshi ni kulinda na kutetea maslahi ya Taifa na mipaka
ya nchi, aidha, Jeshi letu linafanya kazi kwa kufuata mila, desturi, nidhamu,
kanuni na sheria za Kijeshi kwa weledi wa hali ya juu, hivyo lisihusishwe na
propaganda zozote za kisiasa kwani Jeshi letu ni lenye maadili ya kitaasisi ya
hali ya juu.
Jeshi ni taasisi ya dola wala si
taasisi ya kiitikadi, kwa maana uhusiano wake na wanasiasa ni wakati
linapotetea na kulinda maslahi ya wananchi. Inaombwa kuwa makini katika
utoaji wa maelezo au malalamiko, iachwe mara moja vyama vya siasa kuingilia
ratiba za Kijeshi.
Ikumbukwe kwamba tarehe 25 Julai
kila mwaka ni siku ya kuwakumbuka Mashujaa wetu waliolitumikia Taifa hili kwa
umakini na nguvu zote kwa kuleta mafanikio tunayoyaona, na hii ilipitishwa
mwaka 1979 wakati Majeshi yetu yanarudi kutoka Uganda baada ya ushindi wa vita
vya Kagera.
Sherehe ya mapokezi hayo
yalifanyika mji wa Bunazi Wilaya ya Misenye wakati huo Wilaya ya Bukoba Mkoani
Kagera ilipoanzishwa kuwa tarehe hiyo iwe siku ya Mashujaa na kupitishwa
Kisheria, ikabaki siku ya tarehe 01 Septemba kuwa ni siku ya kuanzishwa
kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, hivyo jana tulikuwa tunasherekea
siku ya kuzaliwa JWTZ. Ieleweke hivyo na iachwe mara moja kuchanganya shughuli
za Kijeshi na mambo ya Kisiasa, viongozi wa kisiasa wekeni kumbukumbu zenu
vizuri.
Jeshi linasisitiza wanasiasa ni
vizuri wakasoma vema historia ya nchi wanayotaka kuiongoza na wanayoongoza ili
kuepusha upotoshaji, lugha na maneno yanayotolewa na viongozi wa kisiasa wenye
matakwa binafsi kuhusisha shughuli za Jeshi na siasa zao yanatia ukakasi na
kiungulia, awe makini kuongea vitu ambavyo haelewi na kutokuwa makini zaidi
aelewe madhara yanayoweza kutokea kutokana na upotoshaji.
Jeshi letu
linafanya shughuli zake ki weredi.
Imetolewa
na Kurugenzi ya Habari na Mahusiano
Makao Makuu ya
Jeshi, Upanga
S.L.P
9203, Dar es Salaam, Tanzania.
Kwa Mawasiliano
zaidi: 0784-477638

No comments:
Post a Comment