Jeshi la polisi mkoa wa Singida,
linamshikilia askari mgambo mwajiriwa hospitali ya mkoa, MG 7822 Emmanuel
Daghau (42) kwa tuhuma ya kutoa taarifa za uongo juu ya maiti kufufuka ikiwa
kwenye chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya mkoa.
Imedaiwa kuwa uongo huo ulizua
mtafaruku mkubwa kwa ndugu na jamaa wa merehemu Rahel Erasto (28), aliyekuwa
mkazi wa Minga manispaa ya Singida.
Kaimu kamanda wa polisi mkoa wa
Singida, SSP Mayala Towo, alisema tukio hilo limetokea Septemba, 30 mwaka huu,
majira ya alasiri huko katika hospitali ya mkoa mjini hapa.
Akifafanua, kaimu kamanda huyo
alisema kuwa Septemba, 29 mwaka huu Rahel (marehemu) alifikishwa katika
hospitali hiyo ya mkoa, kwa ajili ya kupata huduma za kujifungua salama.
“Kutokana na sababu za kitabibu
Rahel, alishindwa kujifungua kwa njia ya kawaida na hivyo ililazimika kufanyiwa
upasuaji ambapo mtoto wa kiume alitolewa akiwa hai, Lakini mama kwa bahati
mbaya alifariki dunia usiku saa saba Septemba, 30. Mimba hiyo ilikuwa ya kwanza
kwa marehemu Rahel,” alisema kaimu kamanda huyo.
Akifafanua zaidi, alisema kuwa
baada ya Rahel kufariki dunia, mwili wake ulipelekwa mochwari ambapo kesho
yake, ndugu walijikusanya eneo hilo wakijadiliana namna kuuchukua mwili kwa
ajili ya kwenda kuzika.
Alisema kuwa wakati ndugu
wakiendelea kuzungumzia masuala ya mazishi, alijitokeza mlinzi Daghau na
kuwaeleza kuwa ndugu yao huyo, alifariki kutokana na uzembe na kwamba usiku
akiwa kwenye doria za kawaida, alisikia marehemu akipiga chafya na aliposogelea
dirishani, alimwona akiwa amefufuka.
Towo alisema kuwa awali mgambo huyo
baada ya kuhojiwa na Polisi, alikiri kumwona marehemu huyo akiwa amefufuka na
alisikia akipiga chafya. Alikiri kwa maandishi na kuweka saini yake.
Alisema lakini baada ya Emmanuel kubaini
kuwa baadhi ya ndugu wa marehemu na watoa huduma za afya hospitali ya mkoa
kudai kuwa Rahel amefariki dunia kutokana na matatizo ya kawaida ya uzazi na
wala hakufa na kufufuka, alipohojiwa mara ya pili, alikana maelezo yake ya
awali aliyotoa kwa Polisi.
Wifi wa marehemu Rahel, Mary Mpaki,
alikiri kuwa alimsikia mlinzi Emmanuel wakati akiwatangazia waombolezaji kuwa
marehemu amefariki dunia kutoka na uzembe wa madaktari, na kwamba alipelekwa
chumba cha kuhifadhia maiti akiwa hai.
“Kama ndugu wa marehemu ambao baada
ya kufanyiwa upasuaji kuna ndugu ambao walitaka kulala wodini lakini
hawakuruhusiwa.Tuliposikia maneno ya mlinzi huyo, tuliamini kwa asilimia mia
moja maneno yake kwamba Rahel alipelekwa mochwari akiwa bado yu hai,” alisema kwa
masikitiko.
Mary alisema baada ya taarifa ya
mlinzi huyo, walienda moja kwa moja kituo cha Polisi kutoa taarifa hizo za
kusikitisha.
Ndugu wa marehemu ambaye hakutaka
jina lake litajwe, alisema taarifa iliyotolewa na mlinzi kuwa Rahel alifufuka
na kupiga chafya, zitakuwa ni za ukweli kwa sababu Ni mtu mwenye akili, hawezi
kudanganya jambo hilo.
“Tunasikia kwamba mlinzi kala
matapishi yake kwa kitendo cha kukanusha taarifa alizotoa awali kituo cha
Polisi. Kama amefanya hivyo, itakuwa kuna shinikizo amepata hivyo anatafuta
njia ya kujiokoa,”alisema.
Kaimu mganga mkuu wa mkoa,
Dk.Ramadhani Kabala, alikiri kuwepo kwa taarifa hizo na kudai kwa sasa mwili wa
marehemu unaendelea kufanyiwa uchunguzi, ili kutambua kama kweli Rahel
alifufuka na kupiga chafya akiwa ndani ya chumba cha kuhifadhia maiti.
“Ingawa si rahisi binadamu kufufuka
baada ya kufariki dunia, lakini hatuwezi kuzipuuza taarifa hizi za mlinzi. Ipo
timu inaongozwa na daktari bingwa kutoka wiraza ya mambo ya ndani, Dk.Ahmed
Makata inaendelea na uchunguzi wa kina. Kwa hiyo baada ya kumalizika kwa
uchunguzi, tutawaita waandishi wa habari kuwaeleza ukweli ili muweze kuitaarifu
jamii,” alisema Dk.Kabala.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa
Singida, Mhandisi Mathew Mtigumwe, alikiri kupokea taarifa hiyo ya aina yake,
na kwamba zipo timu mbili zinaendelea na kuchunguzi ili ukweli uweze kubainika.
Na Nathaniel Limu, Singida
No comments:
Post a Comment