Serikali inaendelea kuboresha vyanzo vyake vya mapato ili kukusanya kodi
ipasavyo ambapo imepanga kuanzia mwakani nauli zote za mabasi yanayotoa huduma
za usafirishaji abiria mijini maarufu kama daladala kutoa risiti za
kielektroniki kwa abiria wao.
Imesema
lengo la mpango huo ni ili kubaini kipato halisi cha wamiliki wa mabasi hayo na
kuimarisha ukusanyaji kodi.
Kauli hiyo imetolewa jana Jijini
Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Udhibiti wa Usafiri wa Barabarani kutoka Mamlaka
ya Udhibiti wa Majini na nchi Kavu SUMATRA Bw. Johansen Kahatano wakati wa
uzinduzi wa kamapeni ya uvaaji sare kwa madereva daladala nchini.
Amesema kuwa zoezi hilo liko katika
hatua za ukamilishaji na kuanzia mwezi wa kwanza mwakani mfumo huo utaanza
kutumika lengo likiwa kuboresha na kubadilisha uhusiano baina ya mmiliki na
mfanyakazi wa gari.
Amesema malipo hayo yatasaidia
serikali kufikia lengo lake la kuifanya ajira ya udereva kuwa rasmi kama kazi
nyingine kwa kuwa mapato yote yatakuwa yanaonekana serikalini na kuwabana
wamiliki wa magari kutoa ajira za mikataba kwa wafanyakazi wao.
Sambamba na hilo serikali imetoa
muda wa wiki mbili kwa wamiliki wa daladala kununua sare za wafanyakazi wao na
kwa wale watakaokiuka maagizo hayo watafutiwa leseni zao.
Kwa upande wa madereva kwa kupitia
Mwenyekiti wao Bw. Shabani Mdemu amesema wamekubaliana na maagizo hayo kwakuwa
lengo lao ni kwamba serikali ihalalishe kazi ya udereva ili wapate haki zao za
msingi hasa malipo yao ya msingi.

No comments:
Post a Comment