Zamani
ilikuwa ni kawaida kuona wanawake wanatoboa masikio, pua, ili kuvaa aina
mbalimbali za herini na shemeri.
Siku hizi si ajabu kuona wanaume na
wanawake wakijitoboa au kuchorwa alama (tattoo)
sehemu
mbalimbali za miili yao kama kwenye pua, mdomo, ulimi, tumbo, masikio, mikono,
miguu, kwenye kichwa, mapaja, mgongo na hata sehemu za siri yote haya kwa
ajili ya urembo, miila au desturi zao, kutaka kujinasibu na tabaka fulani au
kutaka kuonyesha ubunifu wao(artistic expression).
Kutoboa/kuchorwa mwili kama
kutafanywa na mtaalamu wa kutoboa/kuchora mwili hakuna madhara yoyote ya
kiafya, madhara ya kutoboa/kuchorwa mwili hupatikana pale tu ambapo
kitendo hiki hufanywa na mtu ambaye si mtaalamu na mjuzi wa fani hii bila
kutumia njia salama za kiafya.
Katika utafiti uliofanywa nchini
Marekani na madaktari bingwa wa ngozi (dermatologists) katika chuo
kikuu chaNorthwestern University Feinberg School of Medicine na
kuchapishwa katika jarida la American Journal of Clinical
Dermatology umesema tatizo kubwa la kutoboa/kuchorwa mwili ni
maambukizi (infection) yanayokisiwa kufika asilimia 20 ya
kutoboa/kuchorwa sehemu mbalimbali za mwili.
Maambukizi haya mara nyingi
husababishwa na bakteria na huonekana katika sehemu ya mwili
iliyotobolewa/kuchorwa.Madhara mengine ya kutoboa/kuchorwa mwili ni kuvuja
damu, mzio/aleji, ngozi kuchanika pamoja na ngozi kuwa na baka
au scarring.
Ni mambo gani ya kuzingatia kabla
ya kutoboa/kuchorwa mwili wako?
1.Unatakiwa kujua uwezekano
wako wa kupata maambukizi – Kama tayari una maambukizi au una kidonda
kilichowazi, ni bora ukaacha kutoboa/kuchorwa mwili mpaka utakapopona na kuwa
na afya njema.
Hatari ya kupata maambukizi ni
kubwa kama utatobolewa/kuchorwa na mtu ambaye si mtaalamu na hana ujuzi wa
kufanya kazi hii.
Hakikisha anayekufanyia hivi
awe anafahamu masuala ya kukinga wateja wake na maambukizi ambayo ni pamoja na
kusafisha vifaa vyake kila baada ya kazi, kuvichemsha vifaa hivyo au
kuhakikisha vipo salama na havina bakteria wowote kwa kutumia kemikali za
kusafishia, kuvifunika vifaa hivyo baada ya kuvisafisha na yeye mwenyewe kuvaa
gloves salama(surgical gloves) wakati wa kufanya kazi yake hiyo ili hata
kama ana magonjwa ya kuambukiza asiweze kukuambukiza wewe kwani zipo taarifa
ambazo watu wameambukizwa ugonjwa wa ukimwi au wamepata ugonjwa
wa tetanus wakati wa kutobolewa/kuchorwa miili yao.
2.Hakikisha huna maradhi yoyote
sugu – Kama una maradhi ya kisukari, ni bora ukaepuka kutoboa/kuchorwa mwili
kwani kidonda chake kinaweza kisipone haraka na hatari ya maambukizi kwa
wagonjwa wa sukari iko juu kupitia kwenye vidonda.
3.Fahamu kuhusu uwezo wako wa
kupona – Unatakiwa uwe na ufahamu juu ya uwezo wa mwili wako katika
kupona(healing tendencies) kidonda chochote kile.
Kuna watu wengine wanapopata
mchubuko au kukatika ngozi zao hupona kwa ngozi ile kufanya kama baka na
uvimbe unaojulikana kama keloids
Kama
wewe ni mmoja wa watu wa aina hii basi unahitaji kuepuka kufanya kitendo hiki
cha kutoboa/kuchora mwili wako.
Sehemu ambazo huchukua muda mrefu
kupona baada ya kutoboa/kuchora mwili ni pamoja na kwenye maeneo ya tumboni,
kwenye chuchu na hata sehemu za siri kwa wanawake.
4.Jua maumbile yako-Sio kila ngozi
ya mwanadamu inafaa kwenye kuitoboa/kuchora, mfano, wale wenye ngozi ya
kwenye tumbo iliyoenuka ndio hufaa kutoboa sehemu hii, kama unataka kutoga
ulimi na ulimi huo ni mfupi kutokana na umbile lako, (Tongue with short
frenum) yaani wale wenye mkunjo chini ya ndimi zao na hivyo kufanya
ulimi kuwa mfupi, hawapaswi kutoga ndimi zao.
5.Hakikisha unafanyiwa na mtaalamu
wa fani hii.Wataalamu wa mambo ya kutoboa/kuchora mwili wana uelewa mkubwa wa
maumbile ya mwanadamu na huwa na vifaa vya kuzuia uvujaji wa damu pindi
unapotokea. Pia huwa na ufahamu wa jinsi ya kukulinda na maambukizi .
6.Historia yako ya afya- Wataalamu
wa kutoboa/kuchora mwili wanatakiwa kuchukua historia ya afya ya wateja
wao inayohusisha magonjwa ya moyo, ugonjwa wa kisukari, mzio/aleji, ugonjwa wa
pumu na kadhalika.
Kama unatumia dawa za ugonjwa wowote
ule ni bora ukamweleza mapema mtaalamu huyo kabla hajaanza kukutoboa/kukuchora
mwili wako.
Ili kuzuia uvujaji wa damu kwa
wingi, unashauriwa kuepuka dawa aina ya aspirin angalau kwa wiki moja
kabla ya kutoboa/kuchora mwili wako, pia epuka dawa jamii ya Non
Steroidal Anti-Inflammataory Drugs (NSAIDS) kamaibuprofen,
naproxen na kadhalika.
7.Hakikisha vifaa sahihi ndivyo
vilivyotumiwa- Hakikisha ya kwamba vifaa vinavyotumiwa ni vile ambavyo
havina madini ya Nickel, pini zenye ubora na vipachiko vya aina
mbalimbali ambavyo ni vya ubora wa hali ya juu.
Pini na vipachiko vidogo vinaweza
kutoka na kusogea kutoka katika sehemu vilipopachikwa na hivyo kukuletea
madhara makubwa.
8.Mfumo wa maisha- Kipachiko cha
katika maeneo ya tumboni (kitovuni, chini ya kitovu nk) huvutia kwa mwanamke
wenye umri mdogo wa miaka ya ishirini na huleta picha mbaya kwa wanawake wale
waliofikia umri wa miaka thelathini na kuendela.
Unatakiwa uangalie na aina ya
taaluma yako kama inaendana na vitu vya aina hivi, mathalani wewe ni
mwanamume unafanya kazi ya mhudumu wa afya, mwalimu, askari, unafanya
kazi kwenye ofisi, muuzaji bidhaa kwa wateja, mtoa huduma za kijamii, halafu
unavaa herini kwenye masikio, ha! Watu watakuchukuliaje?Hakuna atakaye kuelewa
au kukubali kuhudumiwa na wewe.
Pia angalia kama mila,
desturi, dini yako kama inakubali mambo haya kwani itakuwa jambo la aibu
sana kama utatoga mwili wako bila kuzingatia mazingira unayoishi kwani
binadamu tunaishi kulingana na mazingira yetu.
Hii sio kwa wanaume tu hata kwa wanawake,
kabla ya kutoboa/kuchora sehemu husika zingatia taaluma yako, mila,
desturi,mazingira, dini yako nk.
9.Fuata maelekezo vizuri- Fuata
maelekezo unayopewa vizuri jinsi ya kujikinga na maambukizi baada ya
kutoboa/kuchorwa mwili wako, namna ya kusafisha sehemu husika nk.
10.Fahamu madhara ya
kutoboa/kuchorwa sehemu husika- Fahamu kuhusu madhara ya kutoboa/kuchorwa
sehemu husika kwanza kabla ya kutoboa/kuchorwa ili uweze kujiepusha na madhara
hayo.
Pia unatakiwa ujue sehemu hiyo
unayotoboa/kuchora, kidonda chake kinapona baada ya muda gani na maumivu yake
huchukua siku ngapi kuisha? Hatma ya afya yako ipo mikononi mwako!
Tafakari!
No comments:
Post a Comment