Sababu ya mtandao, Dunia ni kama kijiji kimoja.Mtandao
umekuwa kitu cha muhimu kwenye maisha ya watu wengi sana,mitandao inatufanya
tuwasiliane kwa urahisi na ndugu jamaa na marafiki mbalimbali,inatufanya kupata
taarifa mapema zaidi kuliko vyanzo vingi vya taarifa vya ‘kizamani’ kama
runinga, redio na magazeti,mitandao pia ni chanzo cha ajira kwa watu wengine.
Kwa
Africa pekee mpaka kufikia juni mwaka huu kulikuwa na watumiaji wapatao
339,283,342wa mtandao, Tanzania watumiaji walikuwa ni zaidi ya
7,590,794(chanzo-www.internetworldstats.com) hivyo huwezi dharau uwepo wa
mtandao kwenye maisha ya yetu, ndio maana basi tunashauriwa kuchukua tahadhari
mbalimbali tunapokuwa tunaperuzi kwenye mitandao.
Hapa chini nakupa dondoo kadhaa za
kukusaidia walau kujihadhari na hatari ndogondogo ukiwa kama mtumiaji wa
kawaida wa mtandao
1.Usisambaze taarifa zako ovyo
Kuwa makini unapowasiliana na watu
katika mitandao ya kijamii,na kuwa makini zaidi linapokuja suala la kumpa mtu
taarifa zako nyeti kama akaunti za benki,au password,usidangaanyike na jumbe za
kilaghai kama zinazokutaarifu kushinda bahati nasibu,kupata mkopo au mtu anayetaka
kukupa dili lakini anataka taarifa hizo akuwekee kiasi fulani cha
fedha,asilimia 99 huwa ni matapeli wa mtandaoni
2. Epuka malumbano yasiyo na maana mtandaoni
Moja ya sababu ya kuwa na
mitandao,haswa ya kijamii ni kubadilishana mawazo na mijadala mbalimbali lakini
kama ilivyo kwa imani tofauti tulizonazo,wakati mwingi mawazo huwa
tofauti-wasilisha mawazo yako kwa hoja na sio mihemko,jifunze kukubali
kutokubaliana na mawazo ya wengine kama hamjafikia tamati inayoendana,ni sawa
kila mtu kuamua kuamini anachoamini.
La pili ni kukaa mbali na
wazinguaji wa mtandaoni(Trolls) hawa ni watu ambao aidha hukataa kila kitu kwa
ajili ya ubishi tu au hufanya hivyo kutafuta sifa na ‘likes’ kwa kuonekana
wanaenda tofauti na mawazo ya wengine,hapa hata ukiwa na hoja za maana ni kazi
bure kwani kwao ubishi wa mtandaoni ni kama mchezona zaidi ya yote epuka
matusi,kumbuka kuna sheria za mitandao hivyo unaweza kujikuta mikononi mwa dola
kwa sababu ya malumbano yasiyo na mantiki.
3. Usisambaze taarifa usizojua chanzo chake
Umeamka asubuhi umekutana na
taarifa kwenye kundi la WhatsApp mtu fulani maarufu amekufa,bila kuwa na
uhakika sana unasambaza kwa makundi yako mengine 8 na jamaa zako kadhaa kwenye
simu yako.Unakosea,mtandao ni kama bahari kubwa sana ya taarifa zipo taarifa za
ukweli,za uongo za utanina kadharika,na kwa kukusaidia tu kama hujui kuna
baadhi ya blogu na tovuti ambazo ni maalumu kwa ajili ya kuchapisha taarifa za
utani/uongo(Mfano huzzlers.com)-NDIO,yaani taarifa zote utakazosoma humo ni za
kutunga na kufikirika hivyo unapoona taarifa mpya jiridhishe kuhusu chanzo
chake kabla ya kusambaza kwa wengine na kuendeleza upotoshaji.
4. Chunguza mtu unayewasiliana naye
Kweli mitandao ya kijamii
imetengenezwa kwa ajili ya kukutanishwa na marafiki,wale tunaowajua toka zamani
mashuleni au wapya,lakini kuwa na utaratibu wa kumfahamu mtu unaejuana nae mara
ya kwanza mtandaoni kabla ya kuanza kubadilishana nae taarifa zako muhimu na
nyeti,kumtumia picha zako au za familia,kuna akaunti nyingine za mitandao ya
kijamii ni za watu wanaotumia taarifa za uongo kuonyesha ni mtu au jinsia
fulani kumbe sio hivyo inabidi utumie akili ya kuzaliwa katika kujiridhisha na
uhalisia wa mtu unayewasiliana naye.
5.Kutana kwa tahadhari
Umepata rafiki
mtandaoni,mmewasiliana sana sasa mmekubaliana kukutana uso kwa uso,au
umekubaliana na mtu uliyewasiliana nae kwenye mitandao ya kubadilishana,kununua
na kuuziana vitu mbalimbali.Je,unachukua tahadhari gani?Inashauriwa kuwa makini
sana linapokuja suala la kuamisha mawasiliano ya mtandaoni kuwa ya uso kwa
uso,hakikisha mahali mlipokubaliana kukutana ni sehemu ya wazi au sehemu ya
watu wengi na iliyo bize ili kukusaidia kupata msaada endapo jambo lolote la
tofauti litatokea.
Zingatia muda-epuka kukutana na mtu
unayemuona mara ya kwanza mida ya jioni sana au usiku sana,panga muda wa
asubuhi mpaka mchana,muda ambao inapunguza hatari zozote zisizotegemewa,kama
itawezekana pia jitahidi uwe na mtu wa kukusindikiza kwenye kuonana
huko,anaweza kuwa ndugu au rafiki wa karibu kama inashindikana walau umpe mtu yoyote
wa karibu taarifa za awali kuhusu unapokwenda na unayeenda kukutana nae ili iwe
rahisi kupata msaada inapotokea dharura walau kuna mtu ana taarifa zinazoweza
kusaidia
6. Chunguza jumbe unazotumiwa kabla hujafanya lolote
Unafungua kifaa chako, unapata taarifa
mpya kutoka Facebook..unafungua ni msichana mrembo anaomba urafiki,picha zake
ni machachali na zinatia hamasa,unathibitisha na baada ya dakika kadhaa
anakutumia ujumbe,eti muwasiliane zaidi kupitia anwani pepe au anakuambia
ubofye link fulani kuona picha zake zaidi!Usiingie mtegoni
Yawezekana una rafiki Facebook
aliyeomba samahani kuwa picha na video alizosambaza siku kadhaa zilizopita sio
yeye na kwamba akaunti yake ilidukuliwa?Au Pengine ni wewe yalikukuta hayo?Kwa
kiwango kikubwa ni matokeo ya kubofya link za ajabu ambazo huruhusu programu
mbalimbali kuchapisha taarifa kwenye akaunti yako bila wewe kujua lakini
ulifanya hivyo pale ulipobofya link, picha za ajabu au za taarifa fulani ya
kuvutia.
Mifano hiyo ni kuonyesha jinsi
programu kadhaa za kompyuta zilivyotengenezwa kifasaha kukudangaya kuwa ni kitu
fulani mradi tu ubonyeze kitufe fulani au link,na hapo waendeshaji wa programu
hizo huwa na uwezo wa kuchapisha taarifa kwa niaba yako,kutuma ujumbe na picha
kwa marafiki au tu kuchukua taarifa zako na baadae kuzitumia kwa jinsi wanavyojua
wao.
7. Jua walau virefu kadhaa vya mafaili muhimu unayotumia sana
mtandaoni na kwenye kifaa chako
Je,we ni mpenzi wa muziki,video au
programu za simu na kompyuta?Unajua programu za mfumo wa Windows zina kirefu
gani(Mfano .exe,.msi) vitu hivi ni vya kitaalamu kidogo kwa mtumiaji wa kawaida
ila ni muhimu kujua walau juu juu au kwa uchache,ili kuepusha kuweka faili
ambalo sio katika mfumo wa kifaa chako na kumbe faili hilo ni kirusi au
programu chafu,mfano ma faili ya muziki mengi ni .mp3,.aac,.wav hivyo unapotaka
kupakua faili la muziki na unaona kirefu chake kinaonyesha .exe ambayo unajua
ni kirefu cha faili la programu,achana nalo!yawezekana ni programu
iliyotengenezwa kwa mfano wa na jina la muziki fulani ulioutafuta mtandaoni
kukudanganya ili uweke kwenye mfumo wako.
Kingine cha muhumu ni kupakua ma
faili kutoka vyanzo husika na vinavyojulikana ,kama wewe ni mtumiaji wa android
pakua programu zilizopo playstore au tovuti zenye uhakika,windows vilevile
pakua kutoka windows market na ios(iphone/iPad) kutoka itunes na appstore yao.
8. Usiache taarifa zako kwenye vifaa
Njia pekee ya
kuhakikisha taarifa zako muhimu ziko kwenye mikono salama ni kukaa nazo
mwenyewe tu,hivyo unapouza/gawa simu au kifaa kingine chenye picha zako,ama za
familia au zako za falagha na taarifa nyingine hakikisha umezifuta na kutumia
mfumo wa kufuta simu kuwa kama ilivyonunuliwa(wipe data),usijidanganye
kuuza/kugawa simu na kumwamini unayemuuzia/gawia kufanya kazi hiyo kamwe hii
itasaidia kuhakikisha taarifa zako unabaki nazo na haziendi kwenye mikono isiyo
salama.
Kama ilivyo
kwenye uuuzaji,unaponunua pia au kupokea kifaa kutoka kwa mtu ni muhimu kuondoa
taarifa zake kama bado zipo ili kuondoa mkanganyiko linapotokea jambo
lolote(Mfano aliyekuuzia kafanya uhalifu na taarifa zake za mtandaoni
zimefuatiliwa mpaka ulipo wewe,utaisaidia polisi)
Iwapo una akaunti ya mtandao fulani wa kijamii hutaki kuitumia ni vyema pia kutumia njia iliyowekwa na mtandao husika kufuta,tofauti na kuitelekeza tu na kama akaunti ilidukuliwa na ukafungua mpya,fanya kutoa taarifa katika mtandao husika ili ifungiwe kabisa isije kutumika kwa jina lako kufanya utapeli na mambo mengine ya ajabu.
Iwapo una akaunti ya mtandao fulani wa kijamii hutaki kuitumia ni vyema pia kutumia njia iliyowekwa na mtandao husika kufuta,tofauti na kuitelekeza tu na kama akaunti ilidukuliwa na ukafungua mpya,fanya kutoa taarifa katika mtandao husika ili ifungiwe kabisa isije kutumika kwa jina lako kufanya utapeli na mambo mengine ya ajabu.
Kabla
hujaondoka kwenye kifaa cha jumuiya unachotumia kuperuzi,hakikisha ume log out
ili kuepusha matumizi mabaya kwa wengine watakaokuja na kukuta akaunti yako
bado ipo hewani
9.Toa taarifa za unyanyasaji,udhalilishaji au
utapeli
Inapotokea
picha zako au taarifa zinatumika ndivyo sivyo mtandaoni,umetapeliwa au
unadhalilishwa toa taarifa kwa wahusika,inaweza kuwa kwa mtandao husika kama
jambo lenyewe linahusika huko au kwa chombo kinachosimamia jambo lenyewe(Mfano
TCRA ) hii ni muhimu kwako pamoja na wengine ambao watapona baada ya hatua
madhubuti kuchukuliwa kwa wahusika.
Kumekuwepo na
matukio mbalimbali nchi za jirani na hata hapa nchini ya watu kujiua au
kuuliwa,kudhulika na sababu kuja kujulikana baadaye kuwa ni unyanyasaji
ulioanzia mitandaoni
10.Zingatia utunzaji wa password
10.Zingatia utunzaji wa password
Hakikisha
password yako ina nguvu kwa kuwa na tarakimu angalau sita zikiwa ni
mchanganyiko wa maneno na namba,usitumie password rahisi kama jina lako,jina la
mtu au namba zilizozoeleka kama 123,1234,0000 sababu ni rahisi kukisia au
kudukuliwa.
Usihifadhi
password kwa kuandika kwenye vikaratasi ambavyo ni rahisi kupotea,khifadhi kama
message kwenye simu yako,weka kumbukumbu kichwani au tumia program maalumu za
uhifadhi kama 1password,LastPass zinazokuwezesha kuwa na password kuu moja
unayokumbuka(Master) na nyingine kuzihifadhi kwa urahisi mpaka pale
unapohitaji,program hizi pia hukusaidia kutengeneza password mpya au kubadili
ulizonazo kwa kuzingatia vigezo vyote vya password madhubuti
Kuwa chonjo!
kama jinsi
tunavyosema kuwa mtandao unafanya dunia kuwa kama kijiji kimoja hivyo basi kama
jijiji cha kawaida kilivyo,kuna watu wa aina mbalimbali katika kijiji hichi cha
.com,waongo,matapeli,wezi n.k.Hakikisha unachukua tahadhari muda wote
unapoperuzi.
No comments:
Post a Comment