Licha ya Chama cha Wananchi (CUF)
kujivunia uzoefu wa migogoro, huu wa sasa umeweka rehani majimbo yake tisa ya
ubunge yaliyopo Bara na hatari ya kupoteza mvuto na wafuasi kama ilivyotokea
kwa vyama vingine huko nyuma.
Vyama ambavyo vimewahi kupita
kwenye kipindi kigumu kama inavyopita CUF sasa ni NCCR-Mageuzi, UDP na TLP.
Lakini zaidi mgogoro wa NCCR-Mageuzi ndiyo unaotaka kufanana na CUF japo kwa
mazingira tofauti.
Chama cha UDP kilichopata umaarufu
kwa kauli yake ya ‘kuwajaza mapesa watu’ kwenye Uchaguzi Mkuu wa 1995 kilipata
wabunge wanne ambao ni wengi kulingana na mvuto wa chama kwa wakati huo.
Lakini, chama hicho kilikumbwa na
mgogoro wa uongozi baada ya mwenyekiti wake, John Cheyo kupinduliwa mkutanoni
na nafasi yake kuchukuliwa na Nzugule Amani Jidulamabambasi, ambaye hata hivyo
hakudumu kwenye nafasi hiyo kutokana na Msajili wa Vyama vya Siasa kutomtambua.
Pamoja na msajili kulipinga kundi
lililofanya mapinduzi, chama hicho kilianza kudhoofu na kupoteza mvuto hasa
Kanda ya Ziwa ambapo kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2005 kilipata mbunge mmoja- John
Cheyo- aliyedumu hadi 2010, kwa sasa chama hicho hakina mbunge na kimepoteza
ule mvuto wake wa ‘kuwajaza mapesa watu’.
Augustine Mrema mwanzoni mwa miaka
ya tisini alipojiunga na NCCR-Mageuzi baada ya kutoka CCM alikwenda na wafuasi
wengi na kukiimarisha chama hicho kilichokuwa hakina nguvu ikilinganishwa na
vyama vingine.
Nguvu ya NCCR-Mageuzi ilionekana
kwenye Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995, ambapo Mrema
aliyegombea urais kwa chama hicho alishika nafasi ya pili kwa kupata kura
1,808,616 na kupata wabunge katika majimbo 19 Tanzania Bara.
Matokeo hayo yalimuonyesha Mrema
kuwa tishio kwa chama tawala cha CCM, lakini, baada ya uchaguzi huo mgogoro wa
uongozi ndani ya chama hicho ulianza.
Aliyekuwa mwenyekiti wa chama Mrema
alianza kupambana na katibu mkuu wake Mabere Marando, hadi chama kuwa na ofisi
mbili tofauti, kugawana wajumbe wa baraza la wadhamini, wajumbe wa sekretarieti
na kamati kuu.
Mazingira hayo yanataka kufanana na
mgogoro wa CUF uliopo sasa kati ya Profesa Ibrahim Lipumba kwa upande mmoja na
katibu mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad.
Katika mgogoro wa NCCR wakati huo,
Msajili wa Vyama vya Siasa wa wakati huo, Jaji George Liundi (sasa marehemu),
aliutambua upande wa Marando kiutendaji kwa kuwapa ruzuku bila kutamka
hadharani kwamba anaunga mkono kundi lipi.
Nguvu ya msajili ilimdhoofisha
Mrema na kundi lake kwa kuwa hawakuwa na fedha za kuendesha shughuli za chama,
ndipo akaamua yeye na wafuasi wake kuhamia Tanzania Labour Party (TLP), huku
aki tamka ofisi zote mikoani zilizokuwa za NCCR-Mageuzi zibadilike kuwa za TLP.
Licha ya waliobaki NCCR-Mageuzi
kuonyesha kufurahishwa na uamuzi wa Mrema wa kuondoka, chama hicho kilichokuwa
kikijivunia majimbo 19 ya ubunge, kilianza kudhoofika kwenye Uchaguzi Mkuu wa
mwaka 2000, kwanza hakikusimamisha mgombea urais, pili kilipoteza majimbo 18 ya
ubunge na kubaki na jimbo moja tu la Kifu Gulamhussein Kifu (Kigoma Kusini)
ambalo nalo lilipotea kwa njia ya mahakama.
NCCR-Mageuzi, mbali na kupoteza
wabunge, pia chama hicho kilipoteza wafuasi na umaarufu iliyokuwa nao, hali
ambayo CUF inaonekana kuwa nayo kwa kuwa inapita kwenye njia zile zile.
Hata hivyo, Mrema aliyekuwa
akijivunia mtaji wa kura milioni 1.8 alijikuta akipiga mwereka kwenye uchaguzi
mkuu wa 2000 alipogombea urais kupitia TLP alikoambulia kura 637,115 na wabunge
watano.
Kuonyesha kwamba CUF inapita njia
ya NCCR-Mageuzi katika kudhoofika, sasa chama hicho kimegawanyika lakini mbali
na hivyo Msajili wa Vyama vya Siasa ameibuka hadharani kuunga mkono kundi moja
na sasa ameonyesha dalili za kuwapa nguvu ya fedha.
Hata hivyo, kundi la Profesa
Ibrahim Lipumba linaloungwa mkono na msajili likifanikiwa kupata ruzuku
litakuwa na nguvu, lakini kwa wananchi chama hicho kitapoteza mvuto na kuweka
rehani wabunge wa majimbo tisa wa Bara na madiwani.
Huu ni mgogoro wa tano wa kiuongozi
ndani ya CUF baada ya kupitia katika kipindi kigumu wakati wa James Mapalala,
aliyekuwa mwenyekiti wake wa kwanza, Naila Jidawi, Michael Nyaluba,
aliyeanzisha chama hicho upande wa Bara na Hamad Rashid Mohamed.
Uzoefu wa migogo kwa CUF siyo
kigezo kwamba chama hicho hakiwezi kuwa kama vyama vingine vilivyopoteza mvuto
na kupoteza wabunge na madiwani waliowapata katika uchaguzi uliopita.
Kesi ya wadhamini
Katika hatua nyingine, mchakato wa
Bodi ya Wadhamini wa Chama cha Wananchi (CUF), kupata kibali cha kufungua kesi
dhidi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na wenzake unaanza rasmi leo wakati maombi
yaliyofunguliwa na bodi hiyo yatakapotajwa.
Bodi hiyo ya wadhamini CUF
imefungua maombi hayo Mahakama Kuu Masjala Kuu dhidi ya Msajili wa Vyama vya
Siasa, Mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na Msajili, Profesa Ibrahim
Lipumba pamoja na wanachama wengine wa chama hicho waliosimamishwa uanachama
wao.
Katika maombi hayo namba 75 ya
mwaka 2016, bodi hiyo inaomba kibali cha kufungua kesi dhidi ya Msajili,
Profesa Lipumba na wenzake kadhaa, pamoja na mambo mengine, kupinga uamuzi wa
Msajili kumtambua Profesa Lipumba kama mwenyekiti halali wa chama hicho.
No comments:
Post a Comment