Serikali inakamilisha Muswada
wa Sheria utakaoweka wazi sifa za walimu wakiwamo wa vyuo vikuu, msingi na
sekondari nchini.
Hayo yalisemwa jana na Waziri wa
Elimu, Sayansi , Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako
katika kongamano la kujadili hali halisi ya elimu nchini lililoandaliwa na
walimu wastaafu.
Profesa Ndalichako
alisema serikali pia inaandaa mpango wa kuanzisha chombo
maalum cha kitaaluma kitakachosimamia walimu kwa mujibu wa sheria.
Alisema muswada huo utakapokuwa
tayari utawasilishwa bungeni.
Alisema pamoja na mambo
mengine, utataja sifa za mwalimu mkuu na mkuu wa chuo kuondoa dhana
kwamba ualimu ni kazi ya walimu mazoea.
“Ni lazima kuwe na sheria inayoweka
wazi sifa ya mwalimu mkuu wa chuo kikuu na sifa za kuweza kujiunga na chuo cha
ualimu.
“Siyo kuweka tu sheria
zisizojieleza hali ambayo imesababisha taifa kuwa na wasomi wasiokuwa na sifa.
“Ili tuweze kufikia katika mpango
wa kutoa elimu bora ni lazima tuchukue hatua zinazostahiki kwa manufaa ya taifa
ingawa unapochukua hatua Watanzania wengi wanalalamikia suala hili ila ukweli
utabaki kuwa ukweli.
“Nchi haiwezi kuendeshwa na walimu
wasiokuwa na sifa kwa sababu kitakachozalishwa pia kitakuwa ni mtihani na aibu
kwa nchi.
“Kama kuna mwalimu yeyote ambaye
anajijua hana sifa na amekalia kiti hicho kwa zaidi ya miaka 10 atambue kuwa
hicho kiti atakiacha.
“Serikali hii ya awamu ya tano
hatutaki kuwa na walimu wasiokuwa na sifa, bora kujiengua mwenyewe,”alisema Profesa Ndalichako.
Waziri alisema
changamoto kubwa inayoikabili wizara yake ni utekelezaji wa mipango endelevu ya
wizara ambayo ni mizuri lakini utekelezaji wake ni mdogo kutokana na
kuingiliana kwa mipango ya maendeleo endelevu.
No comments:
Post a Comment