Samsung imetoa wito kwa watu wenye simu aina ya Galaxy Note 7 kuzizima mara moja huku ikifanya uchunguzi kubaini ni kwa nini simu hizo, hata zile ambazo kampuni hiyo ilikuwa imethibitisha kwamba ni salama, zinawaka moto.
Kampuni hiyo ya Korea Kusini imesema itasitisha uuzaji wote wa
simu hizo.
Samsung iliwataka watu waliokuwa wamenunua jumla ya simu 2.5
milioni mwezi Septemba kuzirejesha madukani baada ya wateja wengi kulalamika
kwamba betri za simu hizo zilikuwa zinalipuka.
Walipewa simu mpya ambazo zilidaiwa kuwa salama.
Lakini sasa taarifa zimetokea kwamba hata simu hizo zilizodaiwa
kuwa salama zinashika moto.
Mwanamume mmoja jimbo la Kentucky, Marekani anasema aliamka na
kupata chumba chake cha kulala kimejaa moshi uliotokana na simu mpya ya Note 7
aliyokuwa ameipata baada ya kurejesha ya awali.
Siku chache awali, abiria kwenye ndege moja Marekani walitakiwa
kuondoka kwa dharura ndegeni baada ya simu ya Note 7 kuanza kutoa moshi.
"Kwa sababu usalama wa wateja ni jambo tunalotilia maanani
zaidi, Samsung itawataka wasambazaji wote na wauzaji wake kote duniani
kusitisha uuzaji na pia ubadilishaji wa simu za Galaxy Note 7 uchunguzi
unapoendelea," kampuni hiyo imesema.
"Wateja walio na simu asili za Galaxy Note 7 au simu za
Galaxy Note 7 za kubadilisha, wanafaa kuzizima na kuacha kuzitumia na badala
yake kutumia njia nyingine (kuendelea na shughuli zao)," kampuni hiyo
imeongeza.
Samsung inasema simu zilizoathirika ni takriban 2.5 milioni. Kwa
mujibu wa kampuni hiyo, simu 45,000 za Note 7 zimeuzwa Ulaya, na sana
Uingereza. Zaidi ya asilimia 75 zilikuwa zimebadilishwa na wamiliki wake
wakapewa simu nyingine za Note 7 au mitambo mingine ya Samsung.
Galaxy Note 7 ilitarajiwa na Samsung kuisaidia kushindana na
simu ya Apple iPhone 7. Lakini baada ya matatizo hayo, Samsung imeathirika
pakubwa na hisa zake kushuka. Hisa za Apple upande mwingine zimepanda sana
thamani. Aidha, nembo ya Samsung kama kampuni ya kuaminika imeathirika pakubwa.
Wakala wa kulinda wateja Marekani amewahimiza watu kutotumia
simu za Samsung ambazo wamebadilishiwa.
Mwenyekiti wa usalama katika tume hiyo ya Elliot Kaye amesema
uamuzi wa Samsung wa kuacha kuuza simu hizo ni wa busara.
No comments:
Post a Comment