Afisa mkuu zaidi wa chama cha
Republican aliyechaguliwa amesema hatamtetea tena mgombea urais wa chama hicho
Donald Trump, baada ya matamshi yake kuhusu wanawake ambayo yamezua utata.
Spika wa Bunge la Wawakilishi Paul Ryan ameapa kuangazia sasa
kuhakikisha wagombea wa chama hicho wanatetea viti vyao katika Bunge la
Congress.
Hata hivyo, hajabatilisha uamuzi wake wa kumuidhinisha mgombea
huyo.
Bw Trump naye amemjibu Bw Ryan kupitia mtandao wa Twitter na
kusema hafai kupoteza wakati akimpigania.
Awali, mpinzani wa Bw Trump kutoka chama cha Democratic Hillary
Clinton ametilia shaka hatua ya Bw Trump kuomba radhi kutokana na matamshi hayo
aliyoyatoa miaka 11 iliyopita.
Kwenye kadha hiyo ya video, Bw Trump anaonekana akisema
alivyoomba kushiriki mapenzi na mwanamke aliyeolewa. Aidha, anatoa matamshi ya
kudhalilisha kuhusu wanawake.
Lakini Jumapili, Bw Trump alisema maneno yake kwenye kanda hiyo
ya video yalikuwa "mazungumzo ya mzaha faraghani".
Hata hivyo alisema anajutia kuyasema.
Akizungumza wakati wa mdahalo wa urais Jumapili, Bw Trump hata
hivyo alisema hakumnyanyasa mwanamke yeyote kingono.
Bi Clinton aliandika kwenye Twitter Jumatatu kwamba iwapo Bw
Trump anasisitiza msimamo wake, bado inaonesha wazi kwamba "hajajutia
matamshi hayo"
. Bw Trump alipoulizwa kuhusu kanda hiyo ya video kwenye
mdahalo Jumapili, badala yake alimgeukia mpinzani wake Bi Clinton na kusema
mumewe Bill Clinton alikuwa "anawadhalilisha wanawake"
Bi Clinton alikataa kuzungumzia
hilo.
Takriban maafisa 38 wakuu wa chama
cha Republican, wakiwemo masene, wabunge na magavana, wameondoa uungaji mkono
wao kwa Bw Trump, tangu kutokea kwa ukanda huo wa video Ijumaa.
Lakini Jumatatu, mwenyekiti wa
Kamati ya Kitaifa ya Republian Reince Priebus alisema hakuna kitu chochote
kimebadilika kuhusiana na kampeni.
Mgombea mwenza wa Bw Trump, Mike Pence, hata hivyo
amesema ataendelea kumuunga mkono na kumtetea. Hata hivyo awali alikuwa amesema
matamshi ya Bw Trump kwenye kanda hiyo ya video "hayawezi kutetewa".
Lakini akiongea na CNN Jumatatu, bw
Pence alisema "ni heshima kubwa" kwake kumuunga mkono Bw Trump na
akakanusha madai kwamba alitafakari wazo wa kujiondoa.
No comments:
Post a Comment