Kitendo cha askari polisi kumpigia
saluti Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF) anayetambuliwa na Ofisi ya
Msajili wa vyama vya siasa, Profesa Ibrahim Lipumba imezua gumzo la kuhoji
uhalali wake.
Askari huyo alionekana juzi
akimpigia saluti Profesa Lipumba katika eneo la Buguruni ambapo mwanasiasa huyo
alienda kushiriki zoezi la usafi.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Ilala,
Salum Hamduni alipoulizwa kuhusu usahihi wa askari polisi kuwapigia saluti
viongozi wa vyama vya siasa wasio wabunge alijibu kwa ufupi, “sio sawa.”
Kwa mujibu wa Kanuni za Jeshi la
Polisi (PGO) namba 102, haiwataji viongozi wa vyama vya siasa wasio wabunge
kati ya watu wanaopaswa kupewa salamu hiyo ya jeshi yenye kuonesha heshima.
Aliyekuwa Naibu Waziri wa Mambo ya
Ndani wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Kapteni John Chiligati aliwahi kueleza
Bungeni kuwa saluti ni ishara ya kuonesha heshima kwa kiongozi mkuu kwenye
asasi za kijeshi.
Kapteni Chiligati alisema kuwa
mbali na viongozi wa kijeshi, viongozi wengine wanaopaswa kupewa saluti ni wa
mihimili ya Serikali, Bunge na Mahakama.
Wengine ni majaji wote, wabunge,
wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na mahakimu wa mikoa na wilaya wakiwa kwenye
mahakama zao.
Katibu Mkuu wa Chama Cha CCK,
Renatus Muabhi alisema kuwa huenda askari huyo alipiga saluti kwa kupaniki
kutokana na maagizo aliyopewa ya kumlinda Profesa Lipumba katika zoezi hilo.
No comments:
Post a Comment