
Rais Dk. John Magufuli,
amemteua aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna
Tibaijuka kumwakilisha katika mkutano wa makazi wa Habitat III unaofanyika
katika mji wa Quito, Ecuador.
Taarifa iliyoituma kwenye mitandao
ya jamii na Profesa Tibaijuka jana, ilisema katika msafara huo
amefuatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Mandeleo ya
Makazi, Dk. Yamungu Kayandabila.
“Hivi sasa niko Geneva, Uswisi kwa
matayarisho nikielekea Quito Ecuador mkutano wa makazi duniani wa HABITAT
III kumwakilisha Rais wetu nikiwa pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya
Ardhi,namshukuru Rais kwa heshima hii kubwa, Sitamuangusha.
Habitat III,ni mkutano wa uamuzi
na mustakabali wa Shirika la Makazi Duniani na agenda ya maendeleo
endelevu ya miji.
“Kama tunavyojua mkutano wa Habita
I ulifanyika Vancouver,Canada mwaka 1976, Habitat II ulifanyika Istanbul,
Uturuki mwaka 1996 na huu Ecuador Marekani ya Kusini 2016,”alisema.
Alisema kila baada ya miaka 20
wakuu wa nchi hukutana kukubaliana namna ya kuendeleza makazi kupitia Shirika
la UNHABITAT ambalo aliwahi kuliongoza kwa miaka 10.
“Rais Magufuli alichaguliwa na
kuongoza Baraza la Uongozi wa shirika hilo (Governing Council) kwa muhula wa
mwaka 2006/2008 alipokuwa Waziri wa Ardhi.
“Wafanyakazi walimpenda kiasi
kwamba alipobadilishwa wizara na kupelekwa Mifugo na Uvuvi karibu iwe
zogo ofisini kwangu wakidai tutayumba.
“Niliwatuliza na kuwaambia
kumbadilisha wizara hakumuondolei uenyekiti wake na kweli aliendelea nao na
kumaliza,”alisema Tibaijuka.
Alisema katika mkutano huo, jambo
kubwa atakalolipigania ni utaratibu wa shirika hilo kuzisaidia nchi
zinazoendelea kama sisi kwa kuzikopesha halmashauri zao fedha za miundombinu,
bila kuilazimisha Serikali kuu kutoa dhamana kwa mikopo hiyo.
Alisema jambo hilo ni la
msingi kwa vile huleta kasi ya maendeleo ingawa huwa
linapingwa na wakubwa wanaotaka kukopa kupitia Serikali kuu ili waibane
kwa kutumia Benki ya Dunia, kitendo ambacho kinachelewesha kasi ya
maendeleo.
“Tutajitahidi kulingana na
maelekezo ya Rais tunayemwakilisha kuhusu msimamo wa nchi yetu na washirika
wake ambao ni nchi za Afrika na za G77 na China,” alisema.

No comments:
Post a Comment