RAIS Dk. John Magufuli, amemwagiza
Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Charles Mwijage kumrudishia
mfanyabiashara maarufu nchini, Said Salim Bakhresa sukari yake iliyozuiwa
bandarini kwa sababu biashara yake ina tija kwa taifa.
Mbali na hayo, Rais pia amelipa
Shirika la Umeme (Tanesco) miezi miwili kufikisha huduma ya umeme katika
kiwanda cha kusindika matunda na kuzalisha juisi cha Bakhresa Food Products Ltd
kilichopo Mwandege wilayani Mkuranga, mkoani Pwani.
Rais alitoa maagizo hayo jana
wakati wa hafla ya uzinduzi wa kiwanda hicho ambapo alisema ameridhishwa na
uwekezaji wa kampuni hiyo.
Sukari hiyo ya Bakhresa ilizuiwa
katika Bandari ya Dar es Salaam pamoja na wafanyabiashara wengine miezi
michache iliyopita wakati Rais Magufuli alipotangaza kusitisha vibali vya
kuagiza sukari kutoka nje kwa madai ya kulinda viwanda vya ndani.
Agizo hilo lilisababisha uhaba
mkubwa wa sukari ambapo ilipanda na kufikia wastani wa Sh 4,500 hadi 6,000
katika baadhi ya mikoa nchini.
“Tena ndugu yangu, nitakupa
eneo ulime miwa ili upate sukari ya viwandani na ya majumbani, tena nitakupa
bure, wewe Bakhresa umenifurahisha sana kwa uwekezaji wako na sukari yako
niliyoizuia bandarini leo namwagiza Waziri Mwijage itoke na upatiwe,”alisema
Rais Magufuli bila kufafanua kiasi gani cha sukari kilichozuiwa.
Aidha Rais alisema kutokana na
uhaba wa sukari unaoikumba Tanzania kwa miaka mingi ni vyema kushirikiana na
wawekekzaji ili kuondokana na tatizo hilo.
Katika tamko lake Rais aliagiza Wizara
ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuipatia kampuni hiyo ya Azam
eneo la ekari 10,000 kwa ajili ya kilimo cha miwa.
“Kupitia kilimo hicho Watanzania
wengi watapata ajira na pia kiwanda kitatumia sukari ambayo ni salama kwa afya
zetu na pia kuongeza upatikanaji wa sukari hapahapa nchini,” alisema.
Kuhusu Tanesco, Rais Magufuli
alisema suala hilo hawezi kulifumbia macho kwakuwa Tanzania ya viwanda
inategemea zaidi upatikanaji wa umeme wa uhakika.
“Saa nyingine inashangaza
kweli, kiwanda kinaanza kujengwa, watu wapo, kinakamilika, watu wapo, kinaanza
kufanya kazi watu wapo, kinaajiri watu wote hawa, wanafunga jenereta lao, tena
makao makuu ya Wizara ya Nishati na Madini ipo kilomita chache kutoka
hapa,”alisema Rais Magufuli.
Rais pia alisema Serikali yake
inaangalia namna ya kukutana na wataalamu kuangalia mfumo mzuri wa
kuwatoza kodi wawekezaji bila usumbufu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya
Bakhresa, Aboubakari Salim alisema kuna urasimu mwingi katika upatikananji wa
maeneo mapya ya kuanzisha viwanda.
“Tasisi za utozaji kodi zimekuwa
nyingi ambapo utendaji wake ni ule ule hivyo zinatupa usumbufu katika utendaji
wetu, tungeomba zipungue ili tufanye kazi kwa ufanisi zaidi,”alisema Salim.
Naye Meneja Mawasiliano wa Kampuni
ya Azam, Hussein Ally, alisema kiwanda hicho kimeweza kutoa ajira 600 kwa
Watanzania, ambapo kati ya hizo wenye ajira za kudumu ni 380.
Kampuni ya Azam ina jumla ya
viwanda 13 ambapo viwanda 11 vipo Dar es Salaam na vingine viwili vipo
Pwani.
Kwa upande wake Waziri wa Viwanda
Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage alisema kuwa uwekezaji uliofanywa na
makampuni ya Bakhresa unasaidia kuchochea kilimo cha matunda na kutoa fursa ya
soko la uhakika kwa wakulima.
No comments:
Post a Comment