Kiongozi wa upinzani nchini Zambia
Hakainde Hichilema pamoja na naibu wake wamefikishwa mahakamani nchini humo
ambapo wameshtakiwa makosa ya uchochezi wa maasi pamoja na kufanya mkutano
kinyume cha sheria.
Wote wamekanusha mashtaka hayo, na wakaachiliwa huru kwa
dhamana.
Mwandhishi wa BBC Meluse Kapatamoyo anasema wawili hao
walitakiwa kulipa dhamana ya $2,500 (£2,000) kila mmoja na wanatarajiwa kurejea
kortini tarehe 19 Oktoba.
Bw Hichilema alipakia picha zake akiwa kortini siku hiyo ya
Alhamisi kwenye ukurasa wake wa Facebook.
Bw Hichilema na naibu wake Geoffrey Bwalya Mwamba walikamatwa
Jumatano na wakalala seli.
Mashtaka hayo yanahusiana na hotuba ya kushtukiza ambayo Bw
Hichilema aliitoa 26 Septemba katika mji wa Mpongwe, katikati mwa nchi hiyo,
shirika la habari la Reuters limesema likinukuu maafisa wa polisi.
Bw Hichilema alishindwa kwenye uchaguzi wa urais mwezi Agosti na
Rais Edgar Lungu ingawa amelalamika kwamba kulitokea udanganyifu.
Juhudi zake za kutaka mahakama ibatilishe matokeo hayo
ziligonga mwamba.
Aliandika kwenye Facebook Alhamisi:
"Kukamatwa kwetu hakutatuzuia kutumia njia nyingine kutafuta haki kuhusu
uchaguzi huu ambao tulipokonywa ushindi."
No comments:
Post a Comment