Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, amempongeza Balozi Prof. Joram Mukama
Biswaro kwa kuteuliwa kuwa Mwakilishi Maalum wa Mwenyekiti wa Kamisheni ya
Umoja wa Afrika na Mkuu wa Ofisi ya Umoja huo Sudan Kusini.
Balozi Prof. Joram Mukama Biswaro
ameteuliwa na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) Dkt. Nkosazana
Dlamini-Zuma na anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Brigedia Jenerali Sara Thomas
Rwambali ambaye amemaliza muda wake.
Katika pongezi hizo Rais Magufuli
amesema Tanzania imepokea uteuzi huo kwa heshima kubwa na ipo tayari kutoa
ushirikiano wowote utakaohitaji kwa Balozi Joram Mukama Biswaro katika
utekelezaji wa majukumu yake.
“Natambua kazi kubwa iliyopo mbele
yako katika nafasi hiyo muhimu ndani ya Umoja wa Afrika (AU), hata hivyo kwa
kutambua uwezo wako, uzoefu wako na uchapakazi wako naamini kuwa utatekeleza
majukumu yako kwa viwango vya hali ya juu na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja
wa Afrika Dkt. Nkosazana Dlamini-Zuma hatajutia uamuzi wake wa kukuteua katika
nafasi hiyo” amesema Rais Magufuli.
Dkt. Magufuli amemtakia heri Balozi
Prof. Joram Mukama Biswaro katika majukumu hayo mapya, na amemshukuru na
kumpongeza Brigedia Jenerali Sara Thomas Rwambali aliyemaliza muda wake kwa
uwakilishi mzuri katika kipindi chake.
Aidha, Rais Magufuli ambaye ndiye
aliyempendekeza Balozi Prof. Joram Mukama Biswaro kushika nafasi hiyo,
amemshukuru Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Dkt. Nkosazana
Dlamini-Zuma kwa kuridhia mapendekezo yake.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais,
IKULU
Dar es Salaam
04 Oktoba, 2016
No comments:
Post a Comment