Baada ya baadhi ya wakazi wa
Kijiji cha Iringa Mvumi katika Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma kuwaua watafiti
wa Kituo cha Udongo na Maendeleo cha Selian Arusha, wakazi wa kijiji hicho
wamehama makazi yao wakihofia kukamatwa na Jeshi la Polisi.
Waandishi wa habari waliofika
kijijini hapo jana na walishuhudia hali ya utulivu kijijini hapo tofauti na
ilivyozoeleka.
Pamoja na wananchi hao kukimbia
makazi yao, taarifa zinasema viongozi wote wa Serikali ya Kijiji hicho
wamekamatwa na polisi wakiwamo Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji, Albert
Chimanga na Diwani wa Kata ya Iringa Mvumi, Robert Chikole.
Mmoja wa wakazi wa kijiji hicho
aliyejitambulisha kwa jina la Michael Kagisi, alisema kitendo cha wananchi
kukimbia kijiji hicho kimesababisha shughuli nyingi za jamii
kusimama na maduka kufungwa.
Kwa mujibu wa Kagisi, hata
wananchi waliobaki kijijini hapo wakisema
hawakushiriki mauaji hayo, ikifika jioni wanakwenda porini kulala.
“Sehemu kubwa ya watu wameyakimbia
makazi yao kwa sababu wanaogopa kukamatwa na polisi, yaani hata shule hazina
wanafunzi kwa sababu wengi wamekimbia na wazazi wao.
“Yaani waliouawa waliuawa kwa
makosa kwa sababu kabla ya kuwapiga, walijitetea na kujitambulisha,
lakini wananchi hawakutaka kuwasikiliza… baada ya kuwaua,
waliwawekea majani na kuwachoma moto ili wafe haraka,” alisema
Kagisi.
Akifafanua, mwananchi huyo alisema
siku ya tukio ulikuwapo mkutano kijijini hapo na mwenyekiti wa kijiji alipata
taarifa kwamba katika eneo la kutengeneza chumvi, kuna gari ambalo walilitilia
shaka kwamba huenda ni majambazi.
“Siku hiyo tulikuwa kwenye mkutano
na baadaye tulimuona mwenyekiti akiwaita baadhi ya vijana na kuwaagiza waende
eneo la tukio.
“Wale vijana walikwenda huko
walipiga simu kijijini kuwaeleza wananchi, kwamba kuna gari la watu ambao
hawaeleweki.
“Taarifa hizo ziliposambaa, wananchi
walihamasishana na kuelekea eneo la tukio.
“Walipofika tu, walianza kuwapiga,
lakini wale watafiti walijieleza kwamba wao siyo majambazi, huku wakiwaomba
wananchi wawapeleke katika ofisi zao za kijiji, lakini wananchi walikataa na
kuendelea kuwapiga hadi walipowaua,” alisema.
Naye Mchungaji wa Kanisa la
Biblia kijijini hapo, Donald Nyambuya, alisema kwa sasa maisha kijijini hapo ni
ya shida kwa sababu huduma nyingi za jamii zimefungwa baada ya watu
kukimbia makazi yao.
Mwinjilisti wa Kanisa la Waadventista
Wasabato (SDA), Jacob Foda, alisema kitendo cha watu kukimbia makazi yao
kimeathiri huduma ya roho kwa kuwa huwa na kawaida kuwatembelea waumini
wake.
Wakati huohuo, simanzi na majonzi,
jana, vilitawala wakati wa kuaga miili ya Watafiti wa Kituo cha Utafiti wa
Udongo na Maendeleo cha Selian mjini hapa.
Watafiti hao waliuawa juzi na
wananchi wa Kijiji cha Iringa Mvumi, wilayani Chamwino, Mkoa wa Dodoma kwa
kukatwakatwa mapanga na kuchomwa moto.
Miili hiyo iliwasili mjini hapa
jana asubuhi kwa gari ikitokea Dodoma na kuingizwa kwenye eneo la wazi la kituo
hicho kilichopo pembeni mwa Uwanja mdogo wa Ndege wa Arusha kwa ajili ya
wafanyakazi kutoa heshima za mwisho.
Shughuli ya kuaga miili hiyo
ilifanyika asubuhi kwa wafanyakazi, jamaa na marafiki kutoa heshima za mwisho
bila majeneza kufunguliwa kwa kuwa imeharibika.
Baadaye ilipelekwa katika
Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru kwa ajili ya kufanyiwa maandalizi ya
kusafirishwa.
Waliouawa katika tukio hilo
walitambuliwa kuwa ni Jaffari Mafuru aliyesafirishwa jana kwenda Mara kwa
mazishi, Theresia Ngume, aliyetarajiwa kuzikwa jana mjini Arusha na dereva wa
gari walilokuwamo, STJ 9570 aina ya Toyota
Hilux, mali ya Kituo cha Utafiti cha Selian, Nikas Magazine, aliyesafirishwa
kwenda Ifakara, Morogoro kwa mazishi.
Watafiti hao waliuawa wakiwa
katika kazi ya mradi unaoandaa taarifa za hali ya udogo kwa nchi nzima.
Akizungumza baada ya kutoa heshima
za mwisho, Mkurugenzi wa Kituo hicho, Januari Mafuru ambaye ni baba mzazi wa
marehemu Jaffari, alisema tukio hilo limemuumiza sana.
Alisema kituo hicho kimekuwa
kikiendesha mradi huo kwa lengo la kuwasilisha taarifa hizo kwa wakulima wadogo
na wataalamu wa kilimo ziweze kuwasaidia wananchi katika kilimo na
hatimaye kuongeza mazao.
“Mradi huu umemaliza utafiti katika
Mikoa ya Kanda ya Kaskazini ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara. Baada ya hapo
kazi nyingine ilikuwa imeanza Kanda ya Kati Dodoma na Singida.
“Wiki iliyopita, tuliandaa watafiti
wanane na magari yao manne kwa ajili ya kwenda mkoani Dodoma kukusanya udongo
kwa ajili ya kuuleta hapa kwenye maabara za Seliani kufanyiwa utafiti kisha
kutoa matokeo yatakayowarudia wakulima,” alisema Mafuru.
Akizungumzia kuwasili kwa watafiti
hao katika Kijiji cha Iringa Mvumi, wilayani Chamwino yalikotokea mauaji hayo,
Mafuru alisema timu zote zilikuwa na barua za utambulisho pamoja na vifaa vya
kazi.
“Timu iliyokuwa Chamwino katika
Kijiji cha Iringa Mvumi, iliwakuta wanawake wakiendelea na shughuli za
kukusanya chumvi na watafiti waliwasilimia na kujitambulisha wametokea
wapi.
“Taarifa tulizonazo ni kwamba,
baada ya kusalimia, watafiti waliacha gari pembeni na kutembelea
maeneo kuchagua udogo.
“Huku nyuma kundi la wale wanawake
lilitoa taarifa kwa viongozi wao kuwa wamevamiwa na wanyonya damu, ndipo
walipotokea watu wakiwa na mashoka na mapanga na kuwashambulia
kabla ya kuwachoma moto,” alisema.
Mtafiti Mwandamizi wa Kituo cha
Selian, Dk. Lameck Makoye, alilaani mauaji hayo na kusema hajawahi kuona wala
kusikia watafiti wakivamiwa wanapokuwa vijijini.
“Naamini Serikali imeona, binafsi
sijawahi kuona tukio la aina hii kwa sababu watafiti wale walikuwa na
vielelezo vyote vinavyowatambulisha.
“Hata mradi waliokwenda kufanya
ulikuwa ni kwa faida ya wananchi wa Kijiji cha Iringa Mvumi kwa vile umelenga
maeneo ya nchi nzima.
“Sisi Kituo cha Utafiti cha Selian
ndiyo tunaoleta maendeleo ya mkulima kwa nchi nzima kwa kufanya utafiti wa
udongo unaomwezesha mkulima alime vipi na atumie mbolea kwa kiwango gani na ya
aina gani,” alisema Dk. Makoye.
Mume wa marehemu Theresia, Jonas
Mjema, akizungumza kwa huzuni kuhusu kuondokewa na mkewe, alisema kabla
ya tukio la mkewe kuchomwa moto, alizungumza naye asubuhi kujua anaendeleaje.
“Niliwasiliana naye asubuhi
Jumamosi tukatakiana kazi njema, ilipofika jioni nilimtafuta lakini simu yake
haikupatikana.
“Nilijipa matumaini labda
mawasiliano hayakuwa mazuri kwa vile shughuli zao ni za porini.
“Ilipofika Jumapili, nilipigiwa
simu na shemeji yangu akinipa taarifa za tukio la kuchomwa moto mke wangu,” alisema
Mjema aliyeachwa na watoto wawili.
No comments:
Post a Comment