Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea
amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam
akikabiliwa na mashitaka ya kuandika makala ya kupotosha na kusababisha hofu
kwa jamii.
Kubenea, ambaye ni mbunge kwa tiketi
ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alifikishwa mahakamani hapo
jana na kusomewa mashitaka na Wakili wa Serikali, Dereck Mukabatunzi mbele ya
Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri.
Wakili Mukabatunzi alidai kuwa
Julai 25, mwaka huu katika Mtaa wa Kasaba, Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es
Salaam, Kubenea alichapisha habari ya uongo inayoweza kusababisha hofu na
taharuki kwa jamii au kuondoa amani.
Inadaiwa Kubenea alichapisha makala
hiyo kwenye gazeti la Mwanahalisi la Julai 25 hadi 31, mwaka huu, lenye namba
349 ISSN: 1832-5432 ikiwa na kichwa cha habari “Yuko wapi atakayeiokoa
Zanzibar”.
Baada ya kusomewa mashitaka,
Kubenea alikana kutenda kosa hilo na upande wa Jamhuri ulidai upelelezi wa kesi
hiyo umekamilika na kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kumsomea mshitakiwa
maelezo ya awali.
No comments:
Post a Comment