WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ametishia kuwafutia usajili baadhi ya
madalali wa ardhi na nyumba, kutokana na utendaji wao unaokiuka sheria wakati
wa uuzwaji wa nyumba.
Kwa mujibu wa Lukuvi, nyumba nyingi
zimekuwa zikiuzwa bila kufanyiwa tathmini ya gharama zake halisi na hata
zilizofanyiwa wahusika wamekuwa hawashirikishwi.
Lukuvi alitoa kauli hiyo jana
jijini Dar es Salaam alipokutana na madalali wa kampuni mbalimbali, ambapo
aliwaeleza malalamiko anayoyapata kutoka kwa wananchi ambao nyumba zao ziliuzwa
kwa utaratibu usioeleweka.
“Madalali mmekuwa mkiuza nyumba
bila kujali thamani ya mali husika na wengine mnauza kwa bei ya chini, wengine
mnauza kwa bei ya deni lile lile, huo ni uonevu wa hali ya juu huku mkitambua
mnaowafanyia ni maskini,”alisema.
Alisema asilimia kubwa wanaokumbwa
na uonevu huo ni wanawake wajane kutokana na kutojua kama mali walizoachiwa na
waume zao kama ziliandikishwa katika mkopo wa benki.
Waziri Lukuvi aliongeza kuwa
madalali wengi wamekuwa wakikiuka sheria za uuzaji wa nyumba pamoja na mali za
masikini kwa bei ya chini, huku wengine wakifanya mnada katika siku za mwisho
wa wiki.
“Madalali wengi wamekuwa wakiuza
mali za watu kwa kisingizio cha amri ya mahakama tena kwa bei ya asilimia 25
badala ya 75 kama sheria inavyotaka huku mkijua kufanya hivyo ni uonevu na
wizi.
“Ninazo taarifa zenu na hata majina
yenu nayajua, nitawafutia usajili na majina yenu kutangazwa katika gazeti la
Serikali,”alisema.
Waziri Lukuvi alisema madalali
wengi wamekuwa wakifanya mnada wa kuuza mali wakati tayari wakiwa wameshapata
wanunuzi na wengine wakiwa wameshatoa fedha za awali.
Alisema amepata malalamiko ya watu
84 kutoka sehemu mbalimbali nchini ambao wameonewa kwa namna moja au nyingine
na madalali wanaoshirikiana na baadhi ya maofisa wa benki kwa kuwauzia au
kuwabomolea nyumba zao kinyume cha utaratibu.
Katika hatua nyingine Waziri Lukuvi
aliwataka madalali hao kupeleka taarifa zote za mali husika kabla ya kupigwa
mnada kwa msajili wa ardhi na nyumba.
No comments:
Post a Comment