WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Bw. Jordan Rugimbana kuchunguza ni kwa nini
Mkuu wa Magereza Mkoa wa Dodoma Bw Antonino Kilumbi amekwenda kutengeneza
madawati kwa watu binafsi badala ya karakana ya Magereza kama ilivyokusudiwa na
Serikali.
Magereza mkoa wa Dodoma ilipewa sh.
milioni 24 na Serikali ili kutengeneza madawati 480 na kila moja lilitakiwa
kugharimu sh. 50,000. Uongozi wa gereza hilo ulitengeneza madawati hayo kwa
watu binafsi ambapo dawa moja limegharimu sh. 70,000.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo
Jumatano, Oktoba 5, 2016 wakati alipotembelea Gereza la Isanga mkoani Dodoma
akiwa kwenye ziara ya kukagua maeneo yanayotoa huduma za jamii mjini hapa.
Alisema kama gereza hilo halikuwa
na uwezo wa kutengeneza madawati hayo kwa nini kazi hiyo wasingeipeleka kwenye
taasisi nyingine ya umma, hivyo amemtaka Mkuu wa Mkoa Bw. Rugimbana kufuatilia
ziada ya sh. 20,000 kwenye utengenezaji wa kila dawati inatoka wapi na
inakwenda kwa nani.
“Nimesikia kwamba mnawachangisha
askari kiasi kilichoongezeka kwenye utengenezaji wa madawati hayo. Ni marufuku
askari kutoa fedha mifukoni mwao kulipia shughuli za Serikali,” alisisitiza.
Serikali imeandaa utaratibu wa
kuwezesha taasisi zake zikiwemo za kijeshi kwa kuzipa kazi ya kutengeneza bidhaa
na miundombinu mbalimbali ikiwemo madawati ili kuyaongezea tija aliongeza
Kwa upande wake Mkuu wa Magereza
Mkoa wa Dodoma Bw. Kilumbi alisema waliamua kupeleka kazi hiyo kwa watu binafsi
kwa sababu hawana vifaa.
Aidha, Waziri Mkuu alimtaka mkuu
huyo wa magereza mkoa kuimarisha kitengo cha ufundi seremala na kuhakikisha
anatumia vizuri nguvu kazi aliyonayo katika kuzalisha bidhaa mbalimbali.
Kuhusu changamoto ya makazi kwa
askari Waziri Mkuu alisema Serikali inatambua na imeweka mkakati wa wa ujenzi
na kwa upande wa askari Magereza wataanzia kwa mkoa wa Dodoma.
Wakati huo huo Waziri Mkuu
alitembelea maduka ya kuuzia bidhaa mbalimbali zikiwemo nguo katika maeneo ya
soko la Sabasaba na Majengo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
No comments:
Post a Comment