Tundu Lissu, Mbunge wa Singida
Mashariki, jana alishindwa kufika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ili
kujibu mashitaka ya uchochezi huku mdhamini wake akiieleza mahakama kuwa, yupo
jijini Mwanza akisimamia kesi ya Esther Bulaya, Mbunge wa Bunda katika Mahakama
Kuu ya Mwanza.
Lissu ambaye pia ni wakili wa
Mahakama Kuu na mwansheria mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
anashitakiwa kwa uchochezi pamoja na washitakiwa wengine ambao ni ni Jabir
Idrissa, mwandishi mwandamizi wa Gazeti la MAWIO, Simon Mkina, mhariri wa
Gazeti hilo na Ismail Mehboob, meneja wa kampuni ya uchapishaji magazeti ya
Flint.
Mdhamini wa Lissu, Ibrahim Hemed,
alitoa taarifa ya kutofika kwa mdhamana wake mahakamani hapo, mbele ya Hakimu
Mkazi Mkuu, Thomas Simba.
Ibrahim alidai kwamba Lissu
amempatia taarifa kuwa ameshindwa kufika kwa sababu yupo kwenye kesi ya
uchaguzi huku Peter Kibatala wakili wa utetezi akiiomba mahakama ipokee taarifa
za Lissu na ikubali kuhairisha kesi hiyo.
“Lissu ni wakili pekee wa
mlalamikiwa Esther Bulaya katika kesi ya uchaguzi,” alisema
Kibatala.
Baada ya kutolewa kwa maelezo hayo,
Hakimu Simba aliiahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 31 mwaka huu.
Katika kesi hiyo Lissu
anaunganishwa kama mshitakiwa kufuatia kunukuliwa akitoa maoni yake katika
habari iliyochapishwa na gazeti la MAWIO ikiwa na kichwa cha habari “Machafuko
yaja Zanzibar.”
No comments:
Post a Comment